1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya amani Yemen kufanyika Disemba

Grace Kabogo
22 Novemba 2018

Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Jim Mattis amesema mazungumzo ya amani yenye lengo la kumaliza vita nchini Yemen yamepangwa kufanyika mwanzoni mwa mwezi ujao wa Disemba nchini Sweden.

https://p.dw.com/p/38hNj
Jemen durch Luftangriffe zerstörte Häuser in Sanaa
Picha: picture-alliance/Photoshot/M. Mohammed

Mattis amesema kwamba mazungumzo hayo yatakuwa kati ya waasi wa Houthi na wawakilishi wa serikali ya Yemen inayoongozwa na Rais Abedrabbo Mansour Hadi na inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa.

Mwezi uliopita Mattis alitoa wito wa kushtukiza wa kusitishwa mapigano Yemen na kuzisihi pande zinazohasimiana kushiriki katika meza ya mazungumzo ndani ya siku 30.

Umoja wa Mataifa wasogeza muda mbele

Umoja wa Mataifa sasa umesogeza mbele muda huo hadi mwishoni mwa mwaka. Kauli hiyo ya Mattis imetolewa wakati ambapo wizara ya mambo ya nje ya Marekani ikisema kuwa mazungumzo ya amani ya Yemen hayapaswi kucheleweshwa zaidi. Mataifa ya Magharibi yanashinikiza kusitishwa kwa vita nchini Yemen na kuanza upya kwa juhudi za amani ili kumaliza mzozo huo uliodumu kwa zaidi ya miaka mitatu.

Mattis amewaambia waandishi habari kwamba Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu zimesitisha operesheni zake karibu na mji muhimu wa bandari wa Hodeidah, licha ya kuwepo mapigano mengine. Aidha, amezipongeza Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu ambazo majeshi yake yanaiunga mkono serikali ya Rais Hadi, kutokana na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika juhudi za kuleta amani.

US-Verteidigungsminister Jim Mattis
Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Jim MattisPicha: picture-alliance/dpa/AP PhotoT. V. Minh

Hayo yanajiri wakati ambapo mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen, Martin Graffiths akiwa amewasili mjini Sanaa kwa mazungumzo na viongozi wa waasi kwa lengo la kuwashinikiza kushiriki katika juhudi za kumaliza mapigano. Hata hivyo, waasi wa Houthi wamerejelea kauli yao kuitaka jumuia ya kimataifa iwahakikishie usalama wao kwa kiasi kikubwa kwamba wataruhusiwa kutumia njia ya anga na bahari.

Kuvunjika kwa mazungumzo yaliyopita

Waasi wa Houthi walishindwa kuhudhuria katika mazungumzo ya amani yaliyofanyika mwezi Septemba nchini Uswisi, hatua iliyosababisha kuvunjika kwa juhudi za kuvimaliza vita vya Yemen.

Marekani imekuwa ikitoa mabomu na silaha nyingine pamoja na msaada wa kijasusi kwa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia ambao unaiunga mkono serikali ya Hadi, lakini hivi karibuni ilisitisha ujazaji mafuta angani katika ndege za kivita za Saudia.

Mashiri ya Umoja wa Mataifa yamesema kuwa hadi wananchi milioni 14 wa Yemen wako katika hatari ya kukumbwa na baa la njaa, iwapo mapigano yataendelea kusababisha kufungwa kwa bandari ya Hodeidah, njia kuu ya kuingizia misaada ya kibinaadamu nchini humo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, DPA, Reuters
Mhariri: Bruce Amani