1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya amani ya Syria yaisha bila maelewano Astana

John Juma
17 Februari 2017

Wanadiplomasia kutoka magharibi wanasema mashambulio ya angani yanayofanywa na vikosi vya Urusi yameitia doa hadhi ya Urusi kama mpatanishi.

https://p.dw.com/p/2XkZS
Kasachstan Syrien Friedensgespräche in Astana
Picha: picture-alliance/abaca/A. Raimbekova

Duru ya pili ya mazungumzo ya amani kwa Syria ilikamilika Alhamisi mjini Astana, Kazakhstan kwa mafanikio machache. Hayo yakijiri, suala la Syria linatarajiwa kuwa miongoni mwa hoja kuu kujadiliwa leo katika mkutano wa mawaziri wa G20 wanaokutana mjini Bonn Ujerumani. 

Wanadiplomasia kutoka magharibi wanasema mashambulio ya angani yanayofanywa na vikosi vya Urusi yamechangia kutia doa hadhi ya Urusi kama mpatanishi.

Juhudi za Urusi zililemazwa na uhasama mkali kati ya pande mbili pinzani za Syria na pia mkanganyiko kati ya waungaji mkono wa pande hizo, ikiwemo Uturuki inayopingwa vikali na rais wa Syria Bashar al-Assad.

Serikali ya Syria imeitaka Uturuki kuwaondoa wanajeshi wake nchini Syria na ifunge mpaka wa nchi hizo mbili ili kuwazuia magaidi. Waasi kwa upande wao wanailaumu serikali ya Syria na Iran kuwa mara kwa mara zinakiuka mkataba wa usitishwaji mapigano huku Urusi pia ikishindwa kuudumisha mkataba huo.

Alexander Lavrentiev ambaye ni mkuu wa ujumbe wa Urusi katika mazungumzo hayo amesema "Kwa mtizamo wa misururu ya mazungumzo haya nitasema itachukua muda mrefu kuileta serikali na upinzani kufanya mazungumzo ya moja kwa moja. Kuna kutoaminiana kati ya pande mbili zinazohusika katika vita vya Syria. Pande zote zinalaumiana mara kwa mara."

Shinikizo kwa Marekani

Waziri wa nchi za nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel na mwenzake wa Marekani Rex Tillerson katika mkutano wa mawaziri wa G20 mjini Bonn
Waziri wa nchi za nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel na mwenzake wa Marekani Rex Tillerson katika mkutano wa mawaziri wa G20 mjini BonnPicha: picture-alliance/dpa/O. Berg

Katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa mataifa yaliyoendelea  kiviwanda na yanayoinukia kiuchumi maarufu kama G-20, waziri wa Marekani Rex Tillerson amekabiliwa na shinikizo kutoka kwa mawaziri wengine kutaka aeleze msimamo wa Marekani kuhusu mzozo wa Syria, kabla ya mazungumzo ya amani ya Geneva.

Pembezoni mwa mkutano huo unaofanyika mjini Bonn, Tillerson alijiunga na kundi la nchi zinazounga mkono upinzani nchini Syria kutaka mazungumzo ili kupata suluhisho ya mzozo huo ambao umedumu kwa miaka sita.

Akiuhutubia mkutano wa Bonn hivi leo waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Marc Ayrault amesema Urusi sharti iishinikize serikali ya Syria iache kuwachukulia wapinzani wote kama magaidi vinginevyo mazungumzo ya Geneva hayatafaulu.

Hayo yakijiri, jeshi la Uturuki limesema kuwa linakaribia kumaliza operesheni ya kuchukua udhibiti wa mji wa al-Bab ulioko kaskazini mwa Syria kutoka kwa kundi linalojiita Dola la Kiislamu.

Uturuki ilianzisha mashambulio ndani ya Syria mwezi Agosti mwaka uliopita kwa kuunga mkono waasi katika juhúdi za kuliondoa kundi hilo katika eneo hilo lililoko karibu na mpaka na hivyo kuzuia wapiganaji wa Kikurdi.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema eneo ambalo sasa litalengwa kwenye mashambulio yajayo ni mji wa Raqqa ambao ndio makao makuu ya IS baada ya kuondolewa katika sehemu ya ngome yake ya Mosul nchini Iraq.

Mwandishi: John Juma/AFP/RTR

Mhariri: Gakuba Daniel