Mazungumzo ya amani ya Mashariki ya Kati yaingia siku ya pili | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 15.09.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Mazungumzo ya amani ya Mashariki ya Kati yaingia siku ya pili

Duru ya pili ya mazungumzo hayo ambayo yanasimamiwa na Marekani, jana yalifanyika Sharm el-Sheikh, Misri na leo yanaendelea mjini Jerusalem, Israel.

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Hillary Clinton, akiwa na Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu (Shoto) na Rais wa Palestina, Mahmoud Abbas mjini Sharm El-Sheikh, Misri.

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Hillary Clinton, akiwa na Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu (Shoto) na Rais wa Palestina, Mahmoud Abbas mjini Sharm El-Sheikh, Misri.

Duru ya pili ya mazungumzo ya ana kwa ana ya kusaka amani ya Mashariki ya Kati leo inaingia katika siku yake ya pili, ambapo Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na Rais wa Mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas wanakutana mjini Jerusalem kujaribu kuutatua mzozo kuhusu ujenzi wa makaazi ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi. Mazungumzo yao yanafuatia yale ya jana katika mji wa Misri wa Sharm el-Sheikh.

Bwana Netanyahu atakutana kwanza peke yake na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Hillary Clinton na kisha baadaye leo Rais Abbas ataungana nao katika mazungumzo ya pande tatu, ambayo pia yatahudhuriwa na Mjumbe Maalum wa Marekani katika Mashariki ya Kati, George Mitchell. Akizungumza leo na waandishi habari mjini Jerusalam, Bibi Clinton amesema viongozi hao wawili watayajadili masuala muhimu yanayosababisha mzozo katika eneo la Mashariki ya Kati.

Mazungumzo ya siku ya kwanza

Netanyahu na Abbas ambao jana walikutana katika mji wa kitalii wa Sharm el-Sheikh, Misri walishindwa kuutanzua mzozo kuhusu ujenzi wa makaazi. Lakini Bwana Mitchell alisema kuwa viongozi hao wawili walijadiliana kuhusu masuala muhimu yanayozitenganisha pande hizo mbili na kwamba wana imani makubaliano ya amani yatafikiwa katika kipindi cha mwaka mmoja.

Muda wa miezi 10 uliowekwa na Israel wa kusitisha kwa muda ujenzi wa makaazi ya Walowezi wa Kiyahudi, unamalizika tarehe 26 ya mwezi huu wa Septemba na Wapalestina wametishia kuyavunja mazungumzo hayo yanayosimamiwa na Marekani ikiwa muda huo hautarefushwa na ujenzi kuanza tena. Mji wa Jerusalem, wakimbizi wa Kipalestina, mipaka ya taifa la baadaye la Palestina na masuala ya usalama, ndio masuala muhimu ambayo viongozi hao wawili wanatakiwa kuyatatua ili kuyalinda mazungumzo hayo ili kufikiwa kwa mkataba wa amani ya kudumu.

Uzinduzi rasmi wa mazungumzo

Mazungumzo ya sasa ya ana kwa ana yalizinduliwa rasmi mwanzoni mwa mwezi huu mjini Washington, Marekani, baada ya kukwama kwa muda wa miezi ishirini. Aidha, vyombo vya habari vya Israel vimetangaza kuwa huenda Bwana Netanyahu akaelekea Washington mwanzoni mwa juma lijalo, huku kukiwa na tetesi kwamba Rais Barack Obama wa Marekani huenda akajihusisha kujaribu kuutatua mzozo unaopamba moto wa ujenzi wa makaazi. Hata hivyo, Bwana Netanyahu alisema kuwa hatorefusha muda wa kusitisha kwa muda ujenzi wa makaazi hayo.

Baada ya Waziri Clinton kumaliza mazungumzo yake mjini Jerusalem, Ramallah na Amman siku mbili zijazo, Bwana Mitchell anapanga kwenda Syria na Lebanon kuendelea na jitihada za kusaka amani zaidi katika eneo hilo. Kwa upande mwingine, mazungumzo hayo ya ana kwa ana kati ya Netanyahu na Abbas yanaweza kukwamishwa na mashambulio yanayoendelea. Jeshi la Israel limesema kuwa wanamgambo wa Palestina katika Ukanda wa Gaza, leo walirusha roketi na mabomu mawili kwenda Israel. Wanamgambo hao wa Hamas wanaolidhibiti eneo la Gaza tangu mwaka 2007 wanayapinga mazungumzo hayo ya amani kati ya Israel na Palestina.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE)

Mhariri:Abdul-Rahman

 • Tarehe 15.09.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PCSc
 • Tarehe 15.09.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PCSc
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com