1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina kuanzishwa rasmi leo Washington

Josephat Charo28 Novemba 2007

Viongozi wa Israel na Palestina wanaanzisha rasmi mazungumzo ya amani hii leo. Kundi la Hamas linapinga vikali matokeo ya mkutano wa Annapolis

https://p.dw.com/p/CTzL
Rais Bush (katikati) waziri mkuu Ehud Olmert (kushoto) na rais AbbasPicha: AP

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice, amesema viongozi wa Israel na Palestina leo wataanzisha rasmi mazungumzo ya amani katika ikulu ya Marekani mjini Washington.

Kuanzishwa kwa mazungumzo hayo kunafanyika baada ya mkutano wa kihistoria kuhusu amani ya Mashariki ya Kati kufanyika mjini Annapolis katika jimbo la Maryland.

Katika mkutano huo viongozi wamekubaliana kwamba taifa huru la Palestina litaundwa kufikia mwishoni mwa mwaka ujao 2008.

Condoleezza Rice amesisitiza maneno yaliyosemwa na rais George W Bush kwamba maswala yote ambayo bado hayajapatiwa ufumbuzi yatatuliwa.

Rais Bush amesema huu ni wakati muafaka kuwadhihirishia Wapalestina kwamba ndoto yao ya kuwa na taifa huru inaweza kufikiwa katika meza ya amani. Aidha kiongozi huyo amesema kwa wakati huu machafuko yanayohubiriwa na wanamgambo wenye itikadi kali ni kikwazo kikubwa kinachozuia kuundwa kwa taifa huru la Palestina.

Rais Bush binafsi amesema amejitolea kwa dhati kutumia muda wake uliosalia kama rais wa Marekani kutafuta suluhisho la mataifa mawili la mgogoro wa Mashariki ya Kati.

Wakati haya yakiarifiwa maelfu ya wafuasi wa kundi la Hamas katika eneo la Ukanda wa Gaza wamefanya maandamano makubwa katika barabara za mjini Gaza kuyapinga matokeo ya mkutano wa Annapolis nchini Marekani.

Kiongozi wa Hamas, Ismail Haniya, amesema makubaliano yoyote yatakayofanywa na rais wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina, Mahmoud Abbas, hayatakubalika.

Haniya, ambaye alitimuliwa na rais Abbas kutoka kwa wadhifa wake wa uwaziri mkuu, amekataa kurejesha uhusiano wa kawaida kati ya Wapalestina na Israel.

Muandamanaji mmoja ameuwawa mjini Hebron huko Ukingo wa magharibi wa mto Jordan wakati machafuko yalipozuka kati ya maafisa wa usalama walio watiifu kwa rais Mamhoud Abbas na wanamgambo wanaomuita msaliti.