1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo kuhusu Opel yavunjika bila mafanikio.

Sekione Kitojo28 Mei 2009

Mazungumzo ya serikali ya Ujerumani na wadau pamoja na wazabuni wanaotaka kuinunua kampuni ya Opel yamemalizika siku ya Alhamis bila mafanikio. Mazungumzo zaidi yatafanyika Ijumaa.

https://p.dw.com/p/HzEI
Maziri wa fedha wa Ujerumani , Peer Steinbrueck, waziri wa uchumi Karl-Theodor zu Guttenberg, na Roland Koch, waziri mkuu wa jimbo la Hesse, wakati wakizungumza na waandishi habari.Picha: AP

Mazungumzo kuhusiana na msaada wa serikali kwa kampuni la kuunda magari la Opel , sehemu ya kampuni iliyokumbwa na matatizo ya Marekani ya General Motors, yamevunjika mapema alfajiri ya kuamkia leo Alhamis mjini Berlin bila kupatikana matokeo, lakini maafisa wa serikali ya Ujerumani wanasema kuwa mazungumzo hayo yataendelea tena kesho Ijumaa.


Maafisa wa Ujerumani wanailaumu wizara ya fedha ya Marekani , wakisema kuwa ghafla ilidai msaada zaidi kutoka serikali ya Ujerumani ili kuweza kuiwezesha kampuni hiyo ya magari kuweza kuendelea kufanyakazi.

Lakini kiongozi mmoja wa chama cha wafanyakazi nchini Ujerumani baadaye aliyasifia mazungumzo hayo, akisema kuwa mkutano huo umedhihirisha kuwa kuna nia ya kuepusha upotevu wa ajira.

Kile ambacho ni muhimu ni kuwa wanasiasa wanania ya kusaidia, amesema Rainer Einenkel, mwakilishi mkuu wa chama cha wafanyakazi wa Opel mjini Bochum.

Amemsifu mzabuni mmoja, kampuni ya kutengeneza vipuri ya Canada ya Magna , kwa kupunguza kiwango cha upunguzaji wa nafasi ya kazi kinachohusiana na mapendekezo yake.

Mkutano huo uliochukua saa nane katika ofisi ya kansela wa Ujerumani Angela Merkel mjini Berlin ulidumu hadi alfajiri ya leo.

Ujerumani inajadiliana na kampuni mama la Marekani la General Motors ili kuchukua udhibiti wa Opel kwa kuteua bodi ya wadhamini na kuipatia kiasi cha Euro bilioni 1.5 ili kuiwezesha kampuni hiyo kuweza kuendelea kufanyakazi hadi pale mmiliki mpya atakapoinunua Opel kutoka GM.

Wakati huo huo , Ujerumani inajadiliana na wazabuni, ambao wanaripotiwa kuwa wanaitarajia serikali kulipa zaidi ya Euro bilioni 5 ili kulipa fidia ya malipo ya akiba ya uzeeni na ajira ya wafanyakazi wa Opel.

Siku ya Jumatano kampuni ya Vauxhall pamoja na vitengo vingine vya kampuni la General Motors vimekuwa sehemu ya kampuni la Opel lililopanuliwa.

Maafisa wa Ujerumani leo yameshutumu mbinu ambazo wamesema hazisaidii za wajumbe wa majadiliano wa wizara ya fedha ya Marekani. Upande wa Ujerumani umesema kuwa wenzao wa Marekani walianza mazungumzo hayo, ambayo yalidumu kwa zaidi ya saa nane, kwa kutoa madai mapya na tarakimu ambazo hawakuzifahamu hapo kabla.

Kampuni la GM limeeleza kuwa linahitaji kiasi cha Euro milioni 300 za ziada, imesema serikali ya Ujerumani.

Waziri wa uchumi Karl-Theodor zu Guttenberg amesema kuwa wawekezaji wanapaswa kufanyia kazi zaidi maombi yao, na anatarajia jibu kutoka Marekani na wazabuni ifikapo Ijumaa.


Akizungumza na waandishi habari, aliishambulia wazi wizara ya fedha ya Marekani, akisema kuwa anashangazwa na mbinu za majadiliano za baadhi ya washiriki, akiongeza kuwa , nafikiri tunaruhusiwa kusema kuwa wizara ya fedha ya Marekani inapaswa kuweka juhudi kubwa zaidi katika kuchagua watu wake wa kufanya majadiliano.

►◄