Mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran yapiga hatua | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.04.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran yapiga hatua

Naibu waziri wa mambo ya nje wa Iran Abbas Araqchi amesema pande zote mbili katika mazungumzo ya mpango wa nyuklia ziko karibu kuafikiana kuhusu masuala kadhaa

Abbas Araqchi amesema pande zote mbili katika mazungumzo hayo zimepunguza tofauti kubwa zilizokuwepo na kuongeza kuwa mazungumzo hayo yanayonuia kuumaliza mzozo wa muda mrefu bado ni magumu.

Duru hii ya hivi punde ya mazungumzo ya kuelekea kutafuta makubaliano kamili kuhusu mpango wa kinyuklia wa Iran yalianza hapo jana mjini Vienna na yanatarajiwa kukamilika baadaye hii leo.

Bado kazi kubwa ipo

Katika taarifa ya pamoja,Waziri wa mambo ya nje wa Iran Javad Zarif na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton wamesema kazi kabambe bado inahitajika kuweza kumaliza tofauti zilizopo kati ya pande zote mbili.

Kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei

Kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei

Afisa mwandamizi wa serikali ya Marekani anayehusika katika mazungumzo hayo amesema mazungumzo hayo yanayoendelea Vienna,Austria, yanajaribu kupiga hatua za kuridhisha kuwezesha kuanza kuandikwa kwa mkataba wa makubaliano kamili tarehe 13 mwezi ujao ambapo duru nyingine inatarajiwa kufanyika.

Iran inatarajiwa na nchi wanachama wa kudumu wa baraza la usalama la umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani kuusitisha kabisa mpango wake wa kinyuklia ili kutuliza hofu kuwa ina dhamira ya kuunda zana za kinyuklia, madai ambayo Iran imekanusha mara kwa mara.

Siku ya Jumatatu waziri wa mambo ya nje wa Marekani Joh Kerry aliwaambia wabunge wa nchi yake kimsingi Iran inaweza kuunda bomu la kinyuklia iwapo ikiamua kufanya hivyo katika kipindi cha miezi miwili.

Makubaliano kamili yatarajiwa Mei

Mwezi Novemba mwaka jana, Iran ilikubaliana na nchi hizo zenye nguvu kupunguza urutubishaji wake wa madini ya Urani kwa kiwango kinachokubaliwa na shirika la kimataifa la kudhibiti nishati ya Atomiki IAEA.

Makubaliano hayo ya Novemba hata hivyo yalikuwa ya muda tu na pande hizo mbili zinatarajiwa kufikia makubaliano kamili kabla ya tarehe 20 mwezi Julai.

Mkuu wa sera za kigeni wa umoja wa Ulaya Catherine Ashton na waziri wa mambo ya nje wa Iran Javad Zarif

Mkuu wa sera za kigeni wa umoja wa Ulaya Catherine Ashton na waziri wa mambo ya nje wa Iran Javad Zarif

Kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei amenukuliwa hii leo akisema Iran inapaswa kuendelea kuzungumza na nchi hizo zenye nguvu zaidi duniani ili kuumaliza mzozo ulioko wa muda mrefu kuhusu mpango wake wa nyuklia lakini bila ya kurudisha nyuma mafanikio yaliyopatikana nchini humo kutokana na mpango huo wa nyuklia.

Khamenei amesema wajumbe wa nchi yake katika mazungumzo hayo wasikubali kushinikizwa kuafikia lolote na kuongeza kuwa Marekani inajua vyema Iran haina nia ya kuunda silaha za kinyuklia.

Iran inataka mazungumzo hayo yafanikiwe ili iondolewa vikwazo ambavyo vimeuathiri vibaya uchumi wake na kurejea kuwa miamba wa kanda.

Mwandishi:Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri: Yusuf Saumu

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com