1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Mazungumzo kuhusiana na mazingira hayafiki popote"

16 Juni 2011

Watalaamu wa masuala ya mazingira wanaohudhuria mkutano katika mji wa Bonn, Ujerumani, wanasema hatima ya makubaliano ya kimataifa juu ya viwango vya kupunguza gesi chafu duniani inakabiliwa na mashaka.

https://p.dw.com/p/11bdm
Mkuu wa Sekreterieti ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa, Christiana Figueres
Mkuu wa Sekreterieti ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa, Christiana FigueresPicha: DW

Wataalamu wanasema kwamba ikiwa muda wa Mkataba wa Kyoto utashindwa kuongezwa zaidi ya mwaka 2012, bila shaka kutaathiri sana mazungumzo kuhusu suala la tabianchi pamoja na wasimamizi wake, yaani Umoja wa Mataifa.

Makamu wa Rais wa Kituo kinachohusika na ufuatiliaji wa masuala ya tabia nchi cha mjini Washington, Elliot Diringer, anasema bila shaka kuporomoka kwa mkataba wa Kyoto ni hali ambayo haiwezi kuepukika.

Makundi yanayojadiliana yanakabiliwa na hali ya kutoweza kupiga hatua za kutosha au hata kutosonga mbele kabisa katika suala hilo. Ikiwa pande hizo zinazojadiliana zitaamua kufikia ukingoni, bila shaka mpango mzima utakuwa katika hali ya kuporomoka.

Kundi la wanaharakati wa Shirika la Uhifadhi wa Wanyamapori Duniani (WWF) katika mkutano wa mazingira wa Cancun, 2010
Kundi la wanaharakati wa Shirika la Uhifadhi wa Wanyamapori Duniani (WWF) katika mkutano wa mazingira wa Cancun, 2010Picha: picture alliance/dpa

Mazungumzo mapya yanayofanyika chini ya mpango wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) yanayomalizika Ijumaa hii (17.06.2011) mjini Bonn, yanalenga kujenga maridhiano miongoni mwa nchi 194 zitakazokutana katika mkutano mwingine wa ngazi ya juu utakaoanza mwezi Novemba 28 hadi Desemba 9 huko Durban, Afrika Kusini.

Katika makubaliano ya mwaka 1997 yaliyotekelezwa kuanzia mwaka 2005, baada ya kufanyika mazungumzo mapana ya sheria, Mkataba wa Kyoto ulizitaka nchi 37 zilizoendelea kiuchumi kupunguza kwa 5% gesi zake kutoka viwandani, ambazo zinaharibu mazingira katika kipindi cha kuanzia mwaka 2008 hadi 2012, ikilinganishwa na mwaka 1990.

Kuvuka kiwango cha kitaifa kilichopitishwa ni hatua ambayo inabeba adhabu kwa nchi husika katika kipindi hicho kilichowekwa.

Hata hivyo, nchi kama Marekani, ambayo ni moja kati ya wahusika wakuu katika Mkataba huo wa Kyoto, haijawahi kuudhinisha mkataba huo.

Rais wa zamani wa nchi hiyo, George W. Bush, alisema Kyoto ni mkataba uliojaa dosari kwa sababu hauhitaji kuzijumuisha nchi kubwa zilizoendelea kiuchumi, ambazo tayari zinachafua mazingira kuendelea kukabiliwa na vizingiti vile vile.

Nchi za Umoja wa Ulaya zinajitahidi kuwa katika mkondo mzuri wa kupunguza gesi chafu, lakini Canada inaelekea kushindwa kufikia lengo lake la kupunguza viwango vyake vya gesi chafu kwa kiasi kikubwa.

Wakati huo huo, China, India, Indonesia na Brazil zinaongoza mataifa ambayo yanayotajwa na Mkataba wa Kyoto kuwa wachangiaji wa chini ya 30% ya gesi chafu jumla inayotolewa duniani ambayo viwango vyake vilipanda mwaka 2010.

Kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya mazingira na sayansi, kama Alden Meyer kutoka Marekani, nchi zinazoendelea zinatoa kipaumbele kuhakikisha kwamba Mkataba wa Kyoto unaendelea kuwepo kwa sababu ni makubaliano pekee ambayo hayalazimishi nchi kisheria kuyafuata.

Mwandishi: Saumu Mwasimba/IPS
Mhariri: Othman Miraji