Mazungumzo juu ya Darfur bila ya waasi muhimu | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 29.10.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Mazungumzo juu ya Darfur bila ya waasi muhimu

Wajumbe kwenye mkutano huo wameanza kutilia mashaka mashauriano ya Sirte kutokana na kususia viongozi kadhaa muhimu wa makundi ya waasi

Kikao cha Libya kiliwekewa matumaini makubwa lakini hali inavyoonekana matarajio ni machache

Kikao cha Libya kiliwekewa matumaini makubwa lakini hali inavyoonekana matarajio ni machache

Wajumbe wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika walisema hakuna sababu ya kuyakatiza mazungumzo ya amani kwa Darfur yaliyoanzishwa rasmi mjini Sirte, Libya, Jumamosi licha kwamba waasi kadhaa walitaka yasimamishwe. Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa, Jan Eliasson alisema Jumapili aliona ishara kadhaa kwamba mkutano huo utaweza kusaidia kumaliza mgogoro wa miaka minne na nusu unaoendelea huko Darfur na uliogharimu maisha ya watu lakini mbili. Bw. Eliasson alikiri kuwa inabidi kuwepo wajumbe wengi zaidi wa waasi. Kwa mujibu wa wanadiplomasia, maafisa wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika wanatarajiwa kusafiri Darfur kwa azma ya kuwashawishi viongozi muhimu wa waasi.

Wito kadhaa za kuwashawishi waasi kushiriki kwenye mkutano zinasikika. Waziri mkuu wa Uingereza, Gordon Brown, alisema: “Huu ni wakati muhimu wa kufanya uamuzi kwa Darfur, nitatoa mwito kwa pande zote husika kushiriki kwenye mazungumzo yanayoendelea Libya.”

Gordon Brown alisifu hatua ya serikali ya Sudan ya kusimamisha mapigano na alitoa mwito kwa pande zote kushiriki katika hatua hiyo.

Jambo hilo pia alilisisitiza waziri wa mambo ya kigeni wa Sudan, Sammani Wassila, na aliongeza kusema: “Tunatafuta suluhisho la matatizo haya pamoja na ndugu zetu walioko kwenye makundi mengine. Tunafikiri kutokuwepo kwao hakutasaidia kwa sababu lengo la mkutano huu ni kuzungumza kwa pamoja na kuwasilisha malalamiko uliyo nayo badala ya kusema ikiwa madai hayajatimizwa basi huji kwenye mkutano.”

Kinachoendelea kuanzia leo ni kipindi cha kushauriana kati ya makundi ya waasi waliojitokeza Sirte na serikali ya Sudan chini ya uwenyekiti wa mpatanishi kabla ya mazungumzo rasmi kuanza. Mjumbe maalum wa Umoja wa Afrika katika mazungumzo haya, Dkt. Salim Ahmed Salim amefahamisha kwamba tarehe kamili ya kuanza kwa mazungumzo ya amani itafikiwa baadaye.

Makundi sita madogo tu ya waasi yalikuja Sirte na kutuma tu wajumbe wasio wa vyeo vya juu. Katika taarifa ya pamoja, makundi haya yaliomba kupewa muda ili kushauriana na yale yaliyobaki nyumbani. Ahmed Ibrahim Diraige, muasisi wa kundi la Muungano wa Kidemokrasi wa Sudan SFDA, lakini hana matumaini makubwa kwamba makubaliano ya amani yataweza kufikiwa. Amesema: “Kutokana na uzoefu wa yale yaliyotokea awali ningependa kuyaamini. Lakini sitaamini hadi pale nitakapoona yametendeka.”

Makundi ya waasi waliopo Sirte yalisema pia yataongeza juhudi zao kuwashawishi ndugu zao wa Darfur washiriki kwenye mkutano ili kuzuia matokeo mengine sawa na yale ya mazungumzo ya Abuja mwaka 2006. Hapo, kundi moja lilitia saini makubaliano na serikali na makundi mawili yalikataa kufanya hivyo. Baada ya hapo waasi waligawanyika katika makundi madogo madogo na mapigano yalizidi kuwa mabaya Darfur.

 • Tarehe 29.10.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/C77Q
 • Tarehe 29.10.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/C77Q

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com