1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

May auomba Umoja wa Ulaya kulegeza msimamo

Bruce Amani
20 Septemba 2018

Viongozi wa Umoja wa Ulaya  wanaokutana mjini Salzburg, watalizingatia suala la Uingereza kujitoa katika Umoja huo, baada ya waziri mkuu wa Uingereza Theresa May kuwaarifu juu ya fikra zake

https://p.dw.com/p/35DCu
Österreich Informeller EU-Gipfel der Staats- und Regierungschefs in Salzburg
Picha: Reuters/L. Foeger

Wakati wa chakula cha usiku jana, May aliwaambia  viongozi wenzake wa Umoja huo kwamba muhimu hivi sasa ni juu ya Umoja huo kutafuta msingi wa pamoja, huku muda ukiyoyoma kupata  makubaliano kuhusu kujitoa kwa Uingereza Machi 29 mwaka ujao.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanajaribu kuamua  ni kwa umbali gani wafikie maridhiano na May ili aweze kuwa na usemi mkubwa nyumbani Uingereza juu ya suala hilo. May hatokuweko leo katika majadiliano hayo yatayohudhuriwa na viongozi wa Umoja wa Ulaya katika mazungumzo ya Uingereza Michel Barnier.

Österreich Informeller EU-Gipfel der Staats- und Regierungschefs in Salzburg
Viongozi wamekubaliana kuandaa mkutano wa kilele NovembaPicha: Reuters/L. Foeger

Hapo jana Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May aliwatolea wito viongozi wa Ulaya kuachana na kile alichokiita 'masharti yasiyokubalika' ya Brexit ambayo amesema yanaweza kuisambaratisha Uingereza. May aliuomba umoja huo kuushughulikia kwa ukarimu mpango wake mahsusi na unaoweza kufanikiwa.

Na kama tutafikia hitimisho la mafanikio basi kama tu Uingereza ilivyoubadili msimamo wake, Umoja wa Ulaya utahitaji kuubadili msimamo wake pia. Lakini nna matumaini kuwa tukiwa na nia nzuri na ujasiri tunaweza kuafikiana kuhusu mkataba ambao ni mzuri kwa pande zote.

Masuala muhimu yanayojadiliwa na wajumbe ni pamoja na mpaka wa Ireland. Bila kufikia makubaliano, sheria za Umoja wa Ulaya hazitatekelezwa Uingereza, na hiyo huenda ikasababisha vurugu.

Suala hapa ni namna ya kuhakikisha kuwa kile kitakachokuwa mpaka pekee wa ardhi wa Uingereza na Umoja wa Ulaya, kati ya Ireland Kaskazini na Ireland, hautasababisha tena mivutano ya siku za nyuma.

Österreich Informeller EU-Gipfel der Staats- und Regierungschefs in Salzburg
May alifanya mazungumzo na Waziri Mkuu wan Ireland Taoiseach Leo VaradkarPicha: Reuters/L. Foeger

May amekataa pendekezo la Umoja wa Ulaya la kuuweka mkoa huo katika umoja wa forodha kama watashindwa kufikia makubaliano ya kuuweka wazi mpaka mzima wa Umoja wa Ulaya na Uingereza, na badala yake kutoa mpango wa forodha wa muda mfupi ambao utaihusisha Uingereza nzima.

Kansela wa Austria Sebastian Kurz amesema leo kuwa viongozi wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana kuandaa mkutano maalum wa kilele mwezi Novemba ili kuukamilisha mpango wa Brexit na Uingereza.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Jean-Claude Juncker anasema makubaliano na Uingereza bado yako mbali. Mada nyingine itakayozingatiwa leo ni pendekezo la Halmashauri Kuu ya Ulaya kuongeza wafanyakazi wa shirika la mipaka ya Ulaya na Walinzi wa Pwani- Frontex, kutoka 1,500 hadi 10,000 ifikapo mwaka wa 2020 na kulipa mamlaka zaidi.

Wakati kimsingi kukiwa na uungaji mkono, kuna wasiwasi kuhusu kama kutanua majukumu kikosi cha walinzi hao kunaweza kuingilia majukumu ya serikali za kitaifa na za mitaa.

Mwandishi: Bruce Amani/
Mhariri: Gakuba, Daniel