May aihakikishia Ireland kuhusu mpaka | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.02.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

May aihakikishia Ireland kuhusu mpaka

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May amewaambia viongozi wa makampuni wa Ireland ya kaskazini anatafuta kufanya mabadiliko  katika makubaliano ya  Brexit, lakini sio kuondoa kabisa kifungu cha mpaka na Ireland.

Akiwania  kupunguza  hofu  juu  ya  kurejeshwa  kwa  vituo vya udhibiti  wa  mipaka  na  ukaguzi  wa  magari, May  amesema  wakati wa  ziara yake  mjini  Belfast  kwamba  serikali  ya  Uingereza  ina nia  ya  dhati  ya  kuzuwia  ujenzi  wa  kivuko cha  upekuzi  katika mpaka  kati  ya  Ireland  ambayo  ni  mwanachama  wa  Umoja  wa Ulaya  na  Ireland  ya  kaskazini  ambayo ni sehemu ya  Uingereza baada  ya  Uingereza  kujitoa  kutoka  Umoja  wa  Ulaya.

Nordirland Belfast Rede Theresa May, Premierministerin

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May akiingia katika mkumbi wa mkutano aliohutubia wafanyabiashara mjini Belfast

Waziri  mkuu  amesema  alifika mjini  Belfast , "kuwahakikishia  nia yake  ya  dhati  kukamilisha  kujitoa  kwa  Uingereza  katika  Umoja wa  Ulaya  katika  hatua  inayohakikisha  kwamba  hakuna kurejeshwa  kwa  ukaguzi  wa  mpakani  kati  ya  Ireland  ya kaskazini  na  Ireland, hali  ambayo  haitabadilika."

"Pia sitaridhia kuivunja  ahadi  yangu  ya  kuilinda  Ireland ya kaskazini kama  sehemu  kamili  ya  Uingereza. Wakati Halmashauri ya  Umoja  wa  Ulaya  ilipopendekeza  kuwapo  na  kituo cha upekuzi, ambacho  kinajumuisha  kuundwa  kwa  mpaka  wa  forodha katika bahari  ya  Ireland,  nilifanikiwa  kulipinga  hilo. Nilipinga kabisa  pendekezo  hilo.

Hali  hii  haitaharibu  tu  Umoja  wa  soko  la ndani  la  Uingereza, ambalo  ni  muhimu  sana  kwa  biashara  katika Uingereza, bali pia na hapa  Ireland  ya  kaskazini. Hali  hiyo  pia itapuuzia wasi  wasi  wa  kweli wa  watu  wengi  juu  ya  kutengwa na sehemu  yote  ya  Uingereza."

Britisches Parlament verhandelt Brexit

Waziri mkuu Theresa May akiwa katika mjadala wa Brexit katika bunge la Uingereza

Pia  amesisitiza  uungaji  mkono  wa  serikali  kwa  ajili  ya makubaliano  yanayojulikana  kama  ya   "Ijumaa  kuu" ,  mkataba  wa mwaka  1998   ambao  kwa  kiasi  kikubwa  ulimaliza  miongo kadhaa  ya  machafuko  katika  Ireland  ya  kaskazini yanayofahamika  kama "matatizo."

Maneno ya  uhakikisho  ya  May  hata  hivyo  hayakumaliza mkanganyiko  uliopo  kuhusu  mpaka  katika  suala  la  Brexit.

Wakati  huo  huo mawaziri  wa  Uingereza  wamefanya  mazungumzo ya  siri  kuhusiana  na  mipango ya  kuchelewesha  Brexit kwa  wiki nane, limeripoti  gazeti  la  Telegraph jana  jioni.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / ape / rtre

Mhariri: Daniel Gakuba