1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

May afikia makubaliano na chama cha DUP

Sekione Kitojo
26 Juni 2017

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May wa chama  cha Conservative amefikia makubaliano na chama  cha  siasa kali za kizalendo leo (26.06.2017)ambayo yanaruhusu vyama hivyo viwili kuunda serikali.

https://p.dw.com/p/2fQ1J
Großbritannien Theresa May mit Arlene Fostervor 10 Downing Street
Picha: Reuters/S. Wermuth

Lakini  kwa upande  mwingine  serikali italazimika kuipatia  Ireland ya  kaskazini  fedha  za  ziada , zaidi  ya  pauni  bilioni  moja. hatua  hiyo imesababisha  mtafaruku  katika  baadhi  ya  duru  kutokana  na historia  ya  chama  hicho ya  mawazo yake yaliyosababisha uharibifu na mauaji.

Makubaliano  hayo  yenye  utata na  chama  cha  Northern Irish Democratic Unionist  yanakuja  baada  ya  May  kulazimika  kupoteza wingi  wake  bungeni  katika  uchaguzi  mapema  mwezi  huu  ambao aliuitisha  ili  kuimarisha  uungwaji  wake  mkono kwa  ajili  ya mazungumzo  ya  nchi  hiyo  kujitoa  kutoka  Umoja  wa  Ulaya mchakato  unaofahamika  kama  Brexit.

Großbritannien Theresa May mit Vertreter der DUP vor Downing Street
Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May(wapili kushoto) akiwa na kiongozi wa chama cha Democratic Unionist Arlene Foster (wa pili kulia)Picha: Getty Images/AFP/D. Leal-Olivas

Chini  ya  masharti ya  makubaliano  hayo, Ireland  ya  kaskazini itapokea  fedha  za  ziada  pauni bilioni  1.0 sawa  na  euro  bilioni 1.1  kutoka  serikali  kuu  katika  muda  wa  miaka  miwili  ili  chama hicho  cha  DUP  kiweze  kukiunga  mkono chama  cha Conservative  cha  waziri  mkuu  May.

Chama  cha  DUP  kimesema  kitaiunga  mkono  serikali  katika  kila kura  ya  kuwa  na  imani  na  kupitisha  bajeti, pamoja  na  kuunga mkono sheria  zinazohusu  Brexit.

Kwa kura  nyingine  zozote bungeni, chama  cha  DUP, ambacho kina  wabunge  10, kimesema  uungaji  wake  mkono  utategemea suala  na  suala.

Makubaliano  hayo  yalitiwa  saini na maafisa  waandamizi  wa chama  cha  Conservative  na  DUP katika  ofisi  ya  waziri  mkuu , wakati  May  pamoja  na  kiongozi  wa  DUP, Arlene Foster wakiangalia.

England Parlament Theresa May
Waziri mkuu wa Uingereza Theresa MayPicha: picture-alliance/empics

"Kufuatia matokeo  ya  uchaguzi na  uwezo tuliopewa na  watu wa Ireland ya  kaskazini, tumekuwa  katika  majadiliano  na  chama  cha Conservative  na Unionist juu  ya  vipi tunaweza  kuiunga  mkono serikali yenye  wingi mdogo ya chama  cha  Conservative bungeni. Leo tumefikia  makubaliano na  chama cha Conservative juu  ya kuiunga  mkono  bungeni. Makubaliano yatafanyakazi  kuweza kuwezesha kuwa  na  serikali imara  kwa  maslahi  ya  Uingereza katika  muda huu muhimu."

Makubaliano yakosolewa

Vyama vya  upinzani  vimeikosoa  haraka  hatua  hiyo, ambapo kiongozi  wa  chama cha  kiliberali, Liberal Democrats Tim Farron aliyaita, 'makubaliano madogo  yasiyo  na  maana.' 

Großbritannien Tim Farron, Liberaldemokraten
Tim Farron kiongozi wa chama cha Liberal Democrats nchini UingerezaPicha: Reuters/D. Staples

Chama chenye balaa  kimerejea, kikisaidiwa  na DUP," amesema katika  taarifa. Waziri  kiongozi  wa  Wales  Carwyn Jones wa chama  kikuu  cha  upinzani  cha  labour ameliita  wazo  hilo  la muungano "laajabu" na "lisilokubalika"  na  kusema  fedha zilizoahidiwa  ni " kifuniko"  cha  kuiweka  serikali  iliyodhoofika ya waziri  mkuu  kuendelea  kubakia  madarakani.

Tovuti  ya  habari  ya  Independent  imesema  May  "analipa gharama kubwa  ili  kung'ang'ania  madarakani".

Chama  cha  Conservative  kina  viti 317  katika  bunge  lenye  viti 650 baada  ya  uchaguzi  wa  Juni 8 na  kinahitaji  uungwaji  mkono wa  chama  cha  DUP  chenye  viti 10 ili  kiweze  kuendelea kutawala.

Makubaliano  hayo  na  chama  cha  DUP pia  yataendelea  kuwa yenye  utata kwasababu  ya upinzani  wa  chama  hicho  dhidi  ya ndoa  za  mashoga  na  utoaji  mimba na  wasi  wasi kwamba yanaweza  kuvuruga  uwiano tete wa  hatua  za  amani  katika Ireland  ya  kaskazini.

Nordirland DUP-Chefin Arlene Foster
Mkuu wa chama cha DUP Arlene FosterPicha: Reuters/C. Kilcoyne

May  amesema  katika  taarifa  hata  hivyo  kwamba "anayakaribisha makubaliano  haya ambayo  yatawezesha  kufanyakazi kwa  pamoja kwa  maslahi ya  Uingereza  Uingereza  yote."

Chama  cha  DUP kiliunga  mkono Uingereza  kujitoa  kutoka  Umoja wa  Ulaya  lakini  kimesisitiza  haja ya  kuiweka  mipaka  na  jamhuri ya  Ireland  wazi , na  Foster amesema  makubaliano  hayo yataunga  mkono  mchakato  wa  Brexit "ambao  unaunga  mkono pande  zote za Uingereza".

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe  / rtre

Mhariri: Josephat Charo