1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

May aanza kampeni ya kuunadi mkataba wa Brexit

Bruce Amani
26 Novemba 2018

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May ataongoza kikao cha baraza la mawaziri na kutoa taarifa bungeni kuhusu mkataba wake mpya wa Brexit aliousaini na Umoja wa Ulaya

https://p.dw.com/p/38tpc
EU-Sondergipfel zum Brexit in Brüssel
Picha: Getty Images/S. Gallup

May amerejea London baada ya kufikia makubaliano na viongozi wa Umoja wa Ulaya katika mkutano wa kilele mjini Brussels jana Jumapili, ambapo pande zote zilisisitiza kuwa hilo ndilo lililokuwa chaguo pekee bora. May alisema hakuna mkataba mwingine unaoweza kujadiliwa ambao utakuwa bora Zaidi ya uliofikiwa jana

"Kuna wale waliosema kuwa haingewezekana kufikia makubaliano ya Brexit yanayozinufaisha pande zote. toka mwanzo nilikataa wazo hilo la kukata tamaa, na nikaanza kutafuta muafaka ambao unakubalika na Uingereza na Umoja wa Ulaya, ambao unaheshimu matokeo ya kura ya maoni na unatuweka katika mkondo wa ufanisi katika siku za usoni wakati tukiwa na uhusiano wa karibu na marafiki na majirani zetu".

Lakini waziri mkuu huyo anakabiliwa na mtihani wa kupata idhini ya wabunge kabla ya kura ya mwezi ujao, huku wabunge kutoka vyama vyote – wakiwemo wa chama chake mwenyewe cha Conservative na washirika wao wa Democratic Unionist – DUP – wakiupinga mswada huo. 

Makubaliano yaliyofikiwa jana yanaiandaa Uingereza kuondoka kwa njia laini kutoka Umoja wa Ulaya mnamo Machi 29, 2019, na kutoa maono ya kuwepo "ushirikiano wa karibu kabisa iwezekanavyo” baada ya hapo.

EU-Sondergipfel zum Brexit in Brüssel
Uingereza na EU walifikia mkataba BrusselsPicha: Reuters/O. Hoslet

Unahusisha masuala ya kifedha, haki za raia, masharti ya kuiweka wazi mipaka ya Uingereza na Ireland na mipango ya kipindi cha mpito cha miezi 21 ya baada ya Brexit.

Mkataba huo mrefu, unaoweza kutekelezwa kisheria unaambatana na tamko fupi la kisiasa linalotoa matumaini ya mahusiano ya usoni, ikiwa ni pamoja na usalama, biashara na uhamiaji

Hadi pale utakapoidhinishwa na mabunge ya Uingereza na Ulaya, pande zote bado zinapanga kuhusu uwezekano mkubwa wa mtikisiko wa Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya bila ya kuwekwa mipango mipya

Chanzo kimoja cha habari kimesema kuwa May mwenyewe amekiri mjini Brussels jana kuwa kwa sasa hana wingi wa kura bungeni kuupitisha mpango wake. Duru hiyo imeongeza kuwa waziri mkuu huyo ameapa kuwaonya wabunge wake waasi kuwa karibu nusu yao wanaweza kupoteza viti vyao katika uchaguzi ujao kama watashindwa kuupitisha mswada wa Brexit.

Sasa ataanza kampeni kali ya nchi nzima ya kuunadi mpango wake – pamoja na madhara ya kutokuwepo na mkataba – kabla ya kura ya wabunge mnamo au karibu na Desemba 12.

Wakati huo huo, Zaidi ya wabunge 80 wa Conservative wametangaza wazi kuwa wananuia kuupinga mswada huo. Upande wa upinzani pia unajiandaa kupambamana. Kiongozi wa chama cha Labour Jeremy Corbyn amesema chama chake kitayapinga makubaliano hayo bungeni na kushirikiana na wabunge kutoka vyama vingine ili kupinga Uingereza kuondoka Ulaya bila mkataba.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Iddi Sessanga