1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa Ulinzi wajadili hatma ya mapambano dhdi ya IS

25 Oktoba 2016

Mapambano yanaendelea Mosul wakati mawaziri wa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani dhidi ya IS ukijadiliana juu ya hatma ya vita hivyo

https://p.dw.com/p/2Rgud
Paris - Verteidigungsminister der Anti-IS-Koalition beraten in Paris
Mawaziri wa Ulinzi wa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani dhidi ya IS wakiwa ParisPicha: REUTERS/C. Platiau

Katika wakati vikosi vya Iraq vikiendelea na mashambulizi mashariki mwa mji wa Mosul kuukomboa mji huo kutoka mikononi mwa kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS, mawaziri wa ulinzi kutoka nchi za muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani kupambana na kundi hilo wanakutana mjini Paris, Ufaransa, kutathimini operesheni yao hiyo. Mkutano huo wa Paris unafanyika huku kukiweko khofu na mvutano kati ya serikali ya Iraq na Uturuki juu ya ushiriki wa Uturuki kwenye vita dhidi ya IS. 

Akizungumza katika mkutano huo wa mawaziri wa ulinzi, Rais Francoise Hollande wa Ufaransa amezitaka nchi zilizopo katika muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani katika kukabiliana na wapiganaji wa IS mjini Mosul, kujiandaa kukabiliana pia na matokeo yatakayosababishwa na kuporomoka kwa mji huo, ikiwa ni pamoja na kurudi tena kwa wapiganaji hao wa itikadi kali.

Hollande amesema hatua ya kuutwaa tena mji huo haijamalizika, kwa hivyo kila mmoja anabidi kutarajia athari zitakazosababishwa na operesheni yao. Tahadhari aliyoitowa Hollande inahusu pia kuanza kushuhudiwa wapiganaji wa kigeni wa jihadi wakirudi nyumbani kwao wakitokea eneo hilo la mapambano.

Maafisa wa ngazi za juu ya Iraq na Marekani wanasema tayari viongozi wa IS  wameanza kujaribu kuukimbia mji huo na kuelekea Syria upande wa eneo wanalolidhibiti.

Katika mapambano yanayoendelea, inaarifiwa kwamba vikosi maalum vya kijeshi vimekuwa vikijikusanya karibu na medani ya mapambano kufungulia njia mashambulizi ya nchi za Magharibi ambayo wanasema yanalenga kuutwaa tena mji wa Tal Afar na kuzifunga njia za kuelekea nchi jirani ya Syria zinazotumiwa na wapiganaji wa IS wanaotoroka Mosul.

Paris | Treffen der Verteidigungsminister der Anti-IS-Koalition in Paris - Francois Hollande
Rais Francois Hollande akizungumza mkutano wa Paris kuhusu vita dhidi ya ISPicha: picture-alliance/dpa/C. Platiau

Vikosi  maalum vya jeshi la kupambana na ugaidi, CTS, viliyadhibiti tena maeneo ya karibu na vitongoji  vya mashariki mwa Mosul, maeneo ambayo ni ngome za mwisho za IS nchini Iraq.

Wakati huo huo, kundi la muungano wa kijeshi linalofahamika kama Hashed al-Shaabi ambalo linahodhiwa na waasi wa Kishia kutoka Iran linajiandaa kwa upande wake kushambulia eneo la magharibi mwa mji huo wa Mosul, ingawa kujiingiza kwake katika operesheni hii kumesababisha mvutano na hasa kutokana na kuwepo idadi kubwa ya Wasunni katika mji huo.

Wairaq wenye asili ya Kikurdi na wanasiasa wa Kisunni wameipinga hatua hiyo ya kundi la Haseed kama pia wanavyoipinga Uturuki kuingia kwenye mapambano hayo. Uturuki ina wanajeshi wake mashariki mwa Mosul na hapo jana iliripoti kuwashambulia wapiganaji wa IS na kuwauwa 17 kati yao, huku ndege zake za kijeshi chapa F-16 zikiwa tayari kuingia vitani wakati wowote, kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Melvut Casuvoglu.

Hata hivyo, licha ya muungano wa kijeshi kukutana jijini Paris hivi leo, si Iraq wala Uturuki zinazohudhuria mkutano huo, huku pakitajwa tafauti kubwa ya kimkakati iliyopo kati ya majirani hao mahasimu kwenye vita dhidi ya waasi.

Mawaziri wa ulinzi wanaokutana, wakiwemo mwenyeji Jean Yves Le Drian wa Ufaransa na mwenzake wa Marekani, Ashton Carter, watajaribu kuzitafutia ufumbuzi tafauti zao kuhusiana na vipaumbele katika operesheni hiyo pamoja na kutathmini vita hivyo dhidi ya IS baada ya zaidi ya miaka miwili ya kuanzishwa mashambulizi ya angani ya vikosi vya muungano wa kijeshi ukiongozwa na Marekani. 

 

Mwandishi: Saumu Mwasimba/AFP/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef