1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa Ulaya wajadili mustakbali wa Kosovo

10 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/CZi8

BRUSSELS

Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wanakutana leo hii mjini Brussels Ubelgiji kujadili mustakbali wa jimbo la Kosovo wakati muda wa mwisho uliowekwa na Umoja wa Mataifa kufikiwa kwa makubaliano juu ya hatima ya jimbo hilo ukiwa karibu kumalizika.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameweka tarehe 10 leo hii kuwa ni muda wa mwisho kwa wasuluhishi kutoka Umoja wa Ulaya,Marekani na Urusi kufikia muafaka kati ya Kosovo na Serbia lakini hadi sasa mazungumzo yao yameshindwa.

Kosovo bado ni jimbo la Serbia lakini viongozi wa Kosovo wa asili ya Albania wametishia kujitangazia uhuru baada ya kumalizika kwa muda huo.

Kwa kuhofia machafuko ya umwagaji damu kutoka kwa Waserbia Jumuiya ya Kujihami ya Mataifa ya Magharibi NATO imesema itaendelea kuweka kikosi chake cha wanajeshi 16,000 huko Kosovo kuzuwiya mapambano yoyote yake ya kikabila.