Mawaziri wa Ujerumani wamekamilisha ziara Tanzania na kuelekea Afrika Kusini | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 09.04.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Mawaziri wa Ujerumani wamekamilisha ziara Tanzania na kuelekea Afrika Kusini

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, ametoa mwito kwa nchi za Afrika Mashariki zisimame kidete katika kupambana na uharamia katika pwani zao.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle ametoa mwito kwa nchi za Afrika Mashariki zisimame kidete katika kupambana na uharamia katika pwani zao.

Waziri Westerwelle amesema hayo nchini Tanzania , kituo cha kwanza cha ziara yake ya siku tano barani Afrika.

Katika ziara yake, waziri wa mambo ya nje Guido Westerwelle anaongozana na waziri wa misaada ya maendeleo, Dirk Niebel.Hii ni ziara ya kwanza ya pamoja ya mawaziri hao barani Afrika.

Baada ya kuitembelea Tanzania leo watakuwa Afrika Kusini. Watamaliza ziara yao ya siku tano barani Afrika kwa kuitembelea Djibouti kwenye pembe ya Afrika.

Lengo la kutekeleza sera ya ufanisi zaidi ya mambo ya nje kwa makubaliano baina ya wizara hizo mbili limewekwa katika mkataba wa serikali ya mseto ya Ujerumani. Lengo hilo ni muhimu hasa kuhusu nchi zinazoendelea na zinazokabiliwa na migogoro ambapo wahisani na wadau wengine wanatekeleza ajenda tofauti.

Barani Afrika pana nchi nyingi kama hizo- vyombo vya habari kwa sasa vinaripoti sana hasa juu ya Somalia, nchi inayozingatiwa katika sera za nje za nchi za Ulaya na za Afrika kadhalika. Suala la Somalia pia limejadiliwa kwenye mazungumzo baina ya waziri Westerwelle na viongozi wa Tanzania.

Matukio ya sasa yanaonyesha jambo moja wazi: umaskini,migogoro katika ugavi wa raslimali,na maendeleo duni ni sababu zinazoweza kuchangia katika kuleta vurumai katika eneo zima.Uharamia unaotendeka kwenye pembe ya Afrika na Ghuba ya Aden ni miongoni mwa mifano.

Maharamia wanaziteka nyara meli ili kudai vitita vya fedha wanazotumia kwa ajili ya kugharimia vita vya nchini Somalia.

Mawaziri wa Ujerumani na wa Tanzania wameeleza wasiwasi wao juu ya mgogoro wa Somalia.

Waziri wa mambo ya nje wa Tanzania, Bernard Membe, amesema,

"Mizizi ya mgogoro wa Somalia hasa ni ya kiuchumi.Na tunatoa mwito kwa jumuiya ya kimataifa ihusiane na Somalia kama inavyohusiana na nchi nyingine ambamo migogoro inazuka. Nchi hizo zinahitaji usalama na mashirika yanayochangia katika kuleta mageuzi.Lakini asasi hizo zifanye kazi nchini Somalia, usalama utahitajika. Na hiyo ndiyo sababu tunatoa mwito kwa nchi zilizoahidi kuchangia askari zipeleke askari hao nchini Somalia. Nchi hizo ni pamoja na Nigeria, Ghana, Malawi na Senegal"

Kwa upande wake, Tanzania ipo tayari kutoa mafunzo kwa polisi wa Somalia kwa msaada wa Ujerumani.

Mawaziri wa Tanzania na wa Ujerumani pia wamejadili suala la uharamia.

Waziri Westerwelle amesema harakati za kupambana na uharamia ni jambo la manufaa kwa wote.

"Ni kwa maslahi ya nchi zetu kuendesha harakati dhidi ya uharamia. Kwani sote tunategemea kuwepo kwa biashara huru duniani inayoleta manufaa kwa kila upande"

Katika ziara yao ya siku tano barani Afrika mawaziri wa Ujerumani wa mambo ya nje, Guido Westerwelle, na wa ushirikiano wa maendeleo, Dirk Niebel, leo wameanza ziara nchini Afrika Kusini.

Mwandishi:Ute Schaeffer/Mtullya, Abdu

Mpitiaji: Miraji Othman

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com