1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa nje wa Umoja wa ulaya wakutana mjini Brussels

Oumilkher Hamidou24 Februari 2009

Mgogoro wa kiuchumi,siasa mpya ya Marekani na mzozo wa mashariki ya kati ni miongoni mwa mada ziliozojadiliwa

https://p.dw.com/p/H08D
Waziri wa nje wa Ujerumani Frank-Walter SteinmeierPicha: AP


Mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa umoja wa Ulaya walikutana jana mjini Brussels.Mada mkutanoni ilihusu ,miongoni mwa mengineyo,mpango wa kufufua uchumi na hali ya Mashariki ya kati.


Mbali na mpango wa kufufua uchumi wa nchi za umoja wa Ulaya,halmashauri kuu ya Umoja wa ulaya inataka kutia njiani mpango ziada.Unatazamiwa kugharimu yuro bilioni tano zitakazoongezwa fedha ambazo hazikutumika za miradi ya mwaka uliopita.Lakini mpango huo unakabiliana na vizingiti vya kila aina,kuna serikali ambazo zinalalamika dhidi ya gharama zenyewe,nyengine zinakosoa miradi yenyewe na kuna nyengine zinazohisi misaada ya kitaifa ya kufufua uchumi inatosha.Mada hii inapangwa kuzungumziwa mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya utakapoitishwa mwezi ujao.


Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier anakumbusha,mbali na mgogoro wa kiuchumi kuna mambo mengine pia:


"Hatustahiki sisi kuyachukulia mambo kijuu juu tuu.Tunabidi kujishughulisha ipasavyo na masuala yanayohusiana na siasa ya nje,yaliyoorodheshwa katika ajenda,tutake tusitake-tukizingatia suala la Afghanistan kwa kutilia maanani sera za utawala mpya wa Marekani,unaotathmini kwa jicho jengine kabisa mkakati wake katika eneo hilo.Yadhihirika kana kwamba  kuna mengi yanayolingana hivi sasa kati ya msimamo mpya wa Marekani na msimamo wetu.Na hii ni fursa nzuri pia kwetu."


Hapo serikali kuu ya Ujerumani inashukuria kuona kwamba utawala mpya wa Marekani unathamini zaidi masuala ya jamii nchini Afghanistan.Tangu mwanzo Ujerumani ilipigania pawepo wezani sawa kati ya shughuli za kijeshi na zile za kijamii na ndio maana ilikua kila kwa mara ikilaumiwa na utawala wa zamani wa Bush.


Mada nyengine katika mkutano huo wa mawaziri wa mambo ya nchi nza nje wa Umoja wa ulaya mjini Brussels ilihusu hali ya mashariki ya kati baada ya mkuu wa chama cha Likud,Benjamin Netanyahu kutwikwa jukumu la kuunda serikali nchini Israel.Netanyahu anapinga kuwepo taifa la Palastina.Waziri wa jamhuri ya Cheki anaeshughulikia masuala ya ulaya,Alexandr Vondra anahofia kishindo kinachoweza kutikisa jukumu la Umoja wa ulaya katika mashariki ya kati.


"Tunaweza kukumbwa na kishindo,lakini tunabidi kuendeleza utaratibu wa amani.Hata kama njia ya kupatikana ufumbuzi wa madola mawili ni nyembamba,hatuwezi kupakata mikono na kusubiri muda mrefu."


Kabla ya mkutano huo wa 27 wa mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa umoja wa ulaya kuanza mjini Brussels,paliitishwa mkutano ambao si wa kawaida wa wawaandishi habari ambapo waziri wa mambo ya nchi za nje wa jamhuri ya Tcheki,mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa ulaya ,Karel Schwarzenberg na mwenzake wa Ufaransa Bernard Kouchner waliwaelezea waandishi habari jinsi uhusiano wao ulivyo mzuri.