1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Janga

Mawaziri wa nje wa EU kukutana kujadili vita vya Ukraine

16 Machi 2026

Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wanakutana leo kujadili vita vya Ukraine na mzozo wa Mashariki ya Kati pamoja na athari zake.

https://p.dw.com/p/5AT44
Brussels 2025 | EU kukutana kujadili Ukraine na Iran
Mawaziri wa nchi za nje wa Umoja wa Ulaya, kukutana kujadili vita vya Ukraine na IranPicha: dts-Agentur/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Andrii Sybiha, anatarajiwa kujiunga na mkutano huo kwa njia ya video kuelezea mahitaji muhimu ya nchi yake katika kujilinda dhidi ya mashambulizi ya Urusi.

Uungaji mkono wa Umoja wa Ulaya kwa Kyiv ulipata pigo mwezi uliopita, baada ya nchi wanachama 27 kushindwa kufikia makubaliano kuhusu hatua mpya za misaada kabla ya maadhimisho ya mwaka wa nne tangu kuanza kwa uvamizi kamili wa Urusi.

Awamu ya 20 ya vikwazo dhidi ya Moscow pamoja na msaada wa kifedha wa euro bilioni 90 bado vimekwama kutokana na upinzani kutoka Hungary na Slovakia.

Wakati huo huo, Tume ya Ulaya imesema Urusi imenufaika na kupanda kwa bei ya mafuta tangu kuanza kwa mzozo unaohusisha Iran, hali iliyoongeza mapato yake ya kila siku kutokana na mauzo ya mafuta.

Mawaziri hao pia wanatarajiwa kuidhinisha vikwazo vipya vinavyolenga maafisa na taasisi za Iran.