1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

160409 Treffen G8 Agrarminister

Charo Josephat21 Aprili 2009

Bado kuna kazi kubwa kufanya kutimiza lengo la milenia la Umoja wa Mataifa

https://p.dw.com/p/Hams
Waziri wa kilimo na uvuvi wa Ufaransa Michel BarnierPicha: AP

Mawaziri wa kilimo wa nchi zilizoendelea kiviwanda za G8 wamezindua mkakati wa kimataifa unaolenga kuimarisha upatikanaji wa chakula duniani. Taarifa hiyo imetolewa kufuatia mkutano wao wa siku tatu nchini Italia uliomalizika leo.

Kwenye ripoti waliyoitoa hii leo kwa jina, "Changamoto ya Kimataifa: Kupunguza tatizo la uhaba wa chakula," mawaziri wa kilimo wa nchi za G8 wamesema ulimwengu bado uko mbali mno kulifikia lengo la milenia la Umoja wa Mataifa la kupunguza idadi ya watu wanaokabiliwa na njaa kwa asilimia 50 kufikia mwaka 2015. Mawaziri hao pia wametoa mwito baada ya mkutano wao kumalizika huko mjini Cision di Valmarino nchini Italia kwamba hatua madhubuti zichukuliwe kuzuia kupanda kwa bei za bidhaa muhimu.

Huku idadi ya wakazi duniani ikiendelea kuongezeka, athari za mabadiliko ya hali ya hewa zikiendelea kuathiri maisha ya binadamu na mzozo wa chakula ukiwa umesahaulika, swali linalojitokeza hivi sasa ni ikiwa binadamu wataweza kumudu maisha kutokana na uhaba wa chakula.

Huku idadi ya wakazi wanaokabiliwa na kitisho cha njaa duniani ikikaribia kufikia bilioni moja mwaka huu, mawaziri wa kilimo wa nchi za G8 zikiwemo Marekani, Japan, Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, Italia, Canada na Urusi, wamekutana nchini Italia kujadili hali ya chakula duniani.

Mawaziri wa kilimo kutoka muungano wa nchi tano zinazoiunukia haraka kiuchumi duniani, Brazil, China, India, Mexico na Afrika Kusini pia wameshiriki kwenye mkutano huo. Wajumbe katika mkutano huo wametaka kuwepo mfumo wa kuhifadhi kwenye maghala ya kimataifa vyakula muhimu.

Waziri wa kilimo wa Ufaransa Michel Barnier amesema mfumo wa kimataifa wa kusimamia maghala ya chakula unatafutwa kukabiliana na walanguzi wanaolenga vyakula msingi, hatua ambayo ameileza kuwa kashfa. Waziri Barnier amesema ulimwengu unahitaji mifumo ya usambazaji wa chakula itakayofanya kazi katika nchi za Umoja wa Ulaya, akiongeza kuwa hakuna sababu ya kutochukua hatua, huku watu bilioni moja wakiteseka kutokana na njaa. Mikakati ambayo imekuwa ikitumika kukabiliana na baa la njaa duniani imeambulia patupu.

Benedikt Haerlin, mwenyekiti wa asasi zisizo za kiserikali zilizoandaa taarifa kuhusu kilimo duniani, anasema ripoti inayochambua hali ya kilimo duniani ambayo imeandaliwa kwa kipindi cha miaka minne na wataalam 580 kutoka nyanja mabalimbali ulimwenguni kote, imebaini kuwa chakula cha kutosha kinazalishwa lakini usambazaji wa chakula hicho unafanywa kimakosa.

"Lazima tuzalishe kutumia njia bora. Na inapowekwa wazi kwamba leo hii bado chini ya nusu ya nafaka inayozalishwa duniani bado inazalishwa kwa ajili ya chakula cha binadamu, na zaidi ya nusu kwa ajili ya wanyama, mafuta yanayotokana na mimea na kwa matumizi ya viwandani, basi itadhihirika wazi kuwa tatizo sio ikiwa tunaweza kuwalisha watu, bali tatizo hasa ni je kuna chakula cha kutosha kule kinakohitajika?"

19.05.2006 Projekt Zukunft Steiner
Achim Steiner, kiongozi wa shirika la UNEPPicha: DW-TV

Kwa upande wake Kiongozi wa shirika la mazingira la Umoja wa mataifa, UNEP, Bwana Achim Steiner, amesema kunahitajika usimamizi bora wa chakula na amewapa wanasiasa changamoto ya kupitisha maamuzi kuhusu ruzuku ya kilimo na matumizi ya ardhi.

“Jambo la pili ambalo lazima litiliwe maanani ni jinsi kilimo kitakavyokuwa siku za usoni. Taarifa ya shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa kuhusu mzozo wa chakula unaosababisha na mazingira iliyotolewa wiki chache zilizopita ilionyesha kwamba kati ya asilimia 30-40 ya chakula kinachozalishwa leo hupotea aidha wakati wa mavuno mashambani au baadaye masokoni ambapo chakula kilichobakia hutupwa mwishoni wa wiki kama vile katika mahoteli na majumbani."

Mawaziri wa kilimo kutoka Argentina, Australia na Misri pia walihudhuria mazungumzo hayo ya siku tatu, pamoja na maafisa kutoka Umoja wa Afrika, shirika la kimataifa la chakula na Kilimo, FAO, na benki ya dunia.

Waziri wa kilimo wa Italia, Luca Zaia, ambaye nchi yake inashikilia urais wa nchi za G8 amedokeza juu ya mivutano kati ya nchi wanachama katika kufikia taarifa ya mwisho ya pamoja.

Ufaransa na Italia zimeunga mkono wazo la kuanzisha maghala ya nafaka ya kimataifa kuzuia kuongezeka kwa bei za vyakula katika siku za usoni, ikiwa ni pamoja na zile zinazoongezeka kutokana na ununuzi wa kubahatisha. Hata hivyo maafisa wameashiria kwamba Marekani na nchi nyingine wanachama wa G8 hazikubaliani na wazo hilo.

Mwandishi: Helle Jepessen/ Charo Josephat

Mhariri: Abdul- Rahman