1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawasiliano ya simu kati ya wanasiasa Tanzania yadukuliwa?

George Njogopa18 Julai 2019

Madai yameibuka Tanzania kuwa mawasiliano ya simu kati ya wanasiasa yanadukuliwa na hatimaye kusambazwa hadharani kupitia mitandao ya kijamii. Je ni kweli? Walengwa ni kina nani? Kwa lengo lipi? Wasusika ni nani?

https://p.dw.com/p/3MGNB
Treffen von Oppositionsführern in Tansania
Picha: DW/S. Khamis

Wanasiasa nchini Tanzania sasa wanajikuta wakiingia katika wakati mgumu baada ya kuzuka mtindo mpya wa mawasiliano yao ya simu kudukuliwa na hatimaye kusambazwa hadharani kupitia mitandao ya kijamii. Hali hiyo imekuwakumba wanasiasa kadhaa hasa wale kutoka chama tawala Chama Cha Mapinduzi, CCM.

Hakuna aliyesalama, ndivyo wanavyoanza kuhisi wanasiasa wengi hasa wale wanaojitokeza hadharani na kuonyesha ukosoaji wao kwa serikali.

Kuzuka kwa mtindo huo kunafungamanishwa na upepo mpya wa kisiasa unaendelea sasa huku waraka uliotolewa hadharani na waliokuwa makatibu wakuu wa CCM, ukitajwa pengine iliyochochea kwa sehemu kuwepo kwa hali hiyo.

Kwa wiki sasa kumekuwa kukisambazwa sauti za mawasiliano ya simu zinazodaiwa kuwa ni za waaandamizi wa chama hicho tawala wakionyesha namna wasivyoridhishwa na hali ya jumla ya mambo inavyoendelea.

Zitto Kabwe ambaye ni kiongozi mkuu wa chama cha ACT Wazalendo anasema ingawa utamaduni wa kudukua simu umekuwa ukijitokeza katika mataifa mengine duniani, lakini kwa jambo hilo kudhihirika Tanzania ni kitendo kinachowaweka kwenye mtego wanasiasa.

Kwa wiki sasa kumekuwa kukisambazwa sauti za mawasiliano ya simu zinazodaiwa kuwa ni za waaandamizi wa chama tawala CCM
Kwa wiki sasa kumekuwa kukisambazwa sauti za mawasiliano ya simu zinazodaiwa kuwa ni za waaandamizi wa chama tawala CCMPicha: AFP/Getty Images/I. Kasamani

Wadadisi wa mambo wanaona kwamba kuna jambo linaloendelea kufukuta ndani CCM, chama kikongwe afrika. Na udukuzi huo kuwalenga zaidi wanasiasa wa chama hicho hasa wale wanaoonekana kuwa na mirengo tofauti kunaashiria juu ya mpasuko unaokinyemelea chama hicho.

Dk Richard Bonaventura Mbunda mhadhiri idara ya siasa na utawala wa umma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anasema pengine haya yanayoshuhudiwa sasa yamechochewa na mageuzi yaliyotangazwa na mwenyekiti wa chama Rais John Magufuli aliyekuja na mkakati wa kukisafisha chama.

Hata hivyo msomi huyo anasema ni jambo linaloshtua kuona udukuzi unaofanywa ukiachiwa na kusambaa katika jamii.

Kumekuwa na sheria zinazotoa ruhusa kwa mamlaka kufanya udukuzi kwa jambo ambalo linahisiwa pengine linaweza kusababisha madhara kwa taifa, kama vike sheria ya ugaidi na sheria ya usalama wa taifa. Hata hivyo, sheria hizo hazitoa mwanya kwa mawasiliano yanayodukuliwa kuacha yakasambawa kwa jamii.