1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawakala wa upinzani washindwa kuingia vituoni

Amina Mjahid
28 Oktoba 2020

Tafrani zimetokea katika baadhi ya vituo vya kupigia kura baada ya mawakala wa upinzani kushindwa kuingia katika vyumba vinavyotumika kupiga kura kwa madai ya kuwepo kwa ukiukwaji wa kanuni za kusimamia shughuli hiyo.

https://p.dw.com/p/3kXLK
Tansania Sansibar Wahlen
Picha: Getty Images/AFP/D. Hayduk

Licha kwamba hali ya utulivu na amani imetawala kwenye vituo hivyo, mawakala wa vyama vya upinzani wanatuhumu kuwepo kwa kile walichokiita njama za makusudi kuwafanya washindwe kutimiza majukumu yao kwa wakati.

Mawakala hao walipangiwa kuwepo katika baadhi ya vituo maeneo ya wilaya ya Kinondoni wamedai mpaka muda wa kupiga kura kuanza nyakati za saa moja walikuwa bado hawajaingia ndani ya vituo.

Haji Ahmed, wakala wa chama cha ACT Wazalendo amesema, walifika katika kituo cha kupigia kura, wakaruhusiwa kuingia ndani lakini baadae walipata baadhi ya kura zimeshapigwa na walipohoji waliambiawa tayari watu wameshapiga kura jambo ambalo hawakulielewa.

Amesema kwa utaratibu uliopo mawakala wanapaswa kufika kwanza, wajaze fomu kabla la zoezi la upigaji kura kuanza. Mawakala wengine waliojitambulisha kutoka kwenye vyama vinne vya upinzani, walisusia kuingia ndani ya vituo kufuatilia uchaguzi huo kwa kile wanachodai ni ukiukwaji wa kanuni za uchaguzi.

Mawakala wasema hawakupata nafasi ya kutimiza wajibu wao

Tansania Sansibar | Wahlen | Bevölkerung geht Wählen
Picha: AFP/Getty Images

Mawakala hao wameendelea kusisitiza kuwa, ingawa walifika mapema katika vituo vyao walivyopangiwa, bado hawakupata fursa ya kutimiza wajibu wao.

Mbali na hayo sehemu kubwa ya wananchi wameonekana kufurahia haki yao ya katiba ya kupiga kura huku wengine wakisema wanaamini wagombea watavuna kutokana na namna walivyonadi sera zao.

Vituo vya kupigia kura vilivyofunguliwa tangu saa moja asubuhi vinatarajiwa kufungwa saa kumi jioni na ndipo kazi ya kuhesabu kura na kujumulisha matokeo itararajiwa kuanza.

Zaidi ya watu milioni 29 wamejiandikisha kushiriki uchaguzi huu ambao ni wa sita kufanyika tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mnamo mwaka 1992.

Mwandishi: George Njogopa/ Dar es Salaam