1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mauaji yanayofanywa na polisi dhidi ya raia nchini Msumbiji yaongezeka.

Scholastica Mazula29 Aprili 2008

Shirika la Kimataifa la Kutetea haki za binadamu -Amnesty Internation, limesema polisi nchini Msumbiji wamekuwa wakiwaua na kuwatesa watu kwa sababu hawahofii kushitakiwa.

https://p.dw.com/p/Dqpi
Rais wa Msumbiji, Armando E. Guebuza, akiwa na marais Festus G. Mogae wa Botswana na rais Horst Koehler.Picha: AP

Naibu Mkurugenzi wa Amnesty Intenation anayeshughulikia masuala ya Afrika, Michelle Kagari, amesema Polisi nchini Msumbiji wamekuwa wakidhani kuwa wana haki ya kuua na polisi viongozi wachache wenye udhaifu wamekuwa wakiachia vitendo hivyo viendelee.

Katika matukio yote ya ukiukwaji wa haki za Binadamu yanayofanywa na polisi yakiwemo mauaji yasiyokuwa na mpangilio hakujawahi kufanyika uchunguzi wowote na hakuna hatua zozote za Kisheria zilizochukuliwa dhidi ya watu hao.

Marise Castro, ni Afisa wa Amnesty International mjini Londan, anasema Shirika hilo limekuwa likijitahidi kuttoa mapendekezo ya kuangaliwa kwa suala hilo lakini hakuna mabadiliko yoyote.

Anafafanua kuwa Idadi ya watu wanaouawa na polisi imekuwa ikiongezeka tangu mwaka 2007 na Kituo cha Amnesty International nchini Msumbiji tangu mwaka huo kimekuwa kikifanya mazungumzo na wakuu wa polisi na Serikali lakini kwa bahati mbaya mpaka sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.

Katika taarifa ya Amnesty iliyopewa jina la "Kibali cha kuua" pia imegusia kuwa polisi nchini Msumbiji walikabiliwa na changamoto kubwa zilizotokana na visa vingi vya uhalifu, mlimbikizo wa kesi za jinai katika mfumo wa sheria ya nchi hiyo na wakati mwingine vitendo vya utumiaji nguvu walivyofanyiwa polisi na wahalifu.

Mambo hayo yaliisababisha polisi kutumia nguvu dhidi ya washukiwa na wahalifu na mara kadhaa kuwaua washukiwa.

Ripoti hiyo imetaja kuuliwa waandamanaji hapo Februari 2008 ambao walikuwa wanaandamana mjini Maputo kupinga nyongeza kubwa ya nauli ya vyombo vya usafiri.

Si chini ya watu watatu waliuliwa na wengine thelathini kujeruhiwa baadhi yao vibaya sana wakiwa na majeraha ya risasi.

Ripoti hiyo imesema kwamba polisi kwa ujumla wamekuwa hawayashughulikii madai ya wananchi, wanatoa habari chacche kwa wale ambao wanalalamika dhidi ya polisi kuendea kinyume haki za binadamu.

Watu walioathirika hawalipwi fidia kwa vitendo walivyofanyiwa.

Bwana Kagari alisema, Afisa yeyote wa polisi anayeshukiwa kuhusika na vitendo dhidi ya haki za binadamu awajibishwe na kwamba maofisa wa polisi lazima watambue kwamba hawawezi kutesa, kuwapiga watu na kuwaua bila ya kuulizwa.

Alisema Polisi lazima wawe na dhamana kutokana na vitendo vyao ikiwa wanataka sura ya kazi yao iwe bora huko Msumbiji.

Hata hivyo Polisi nchini Msumbiji wamekataa kuzungumzia suala hilo.