1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mauaji ya balozi wa Italia yazusha mzozo wa Italia na DRC

Jean Noel Ba-Mweze26 Februari 2021

Mauaji ya balozi wa Italia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yamezusha mvutano kati ya nchi hizo mbili, huku Italia ikitaka uchunguzi na majibu kamili kutoka Umoja wa Mataifa.

https://p.dw.com/p/3px8H
DR Kongo | Luca Attanasio, ermordeter italienischer Botschafter
Picha: FOTOGRAMMA/IPA/picture alliance

Hiyo ni baada ya vyombo vya habari vya Italia kuripoti kuwa Luca Attanasio aliuawa na risasi ya jeshi la Kongo.

Balozi huyo aliyezikwa jana mjini Rome, Italia, aliuawa pamoja na mlinzi wake, raia wa Italia, na pia dereva wa Shirika la Mpango wa Chakula Ulimwenguni, WFP, ambaye ni raia wa Kongo, baada ya msafara wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa kushambuliwa Jumatatu huko Kivu ya Kaskazini. Na sasa, wabunge kadhaa kutoka Beni wanataka uchunguzi ufanyike pia katika eneo lao ili kugundua wadhamini halisi wa mauaji huko.

Mamlaka nchini Italia zinataka kuelewa wazi mazingira ambamo alifariki balozi wake huyo kijana kabisa.

Luca Attanasio pamoja na mlinzi wake Vittorio Lacovacci, ambaye alikuwa pia Mtaliano, na pia dereva Mkongomani, Moustapha Milambo, waliuawa wakiwa katika msafara ulioandaliwa na Shirika la Mpango wa Chakula Ulimwenguni, WFP, na ndiyo sababu ya serikali ya Italia inaunyooshea kidole cha lawama Umoja wa Mataifa.
Soma pia:

Lakini yote yatajulikana na huenda kukawa na mwanga zaidi kuhusu mauaji hayo kulingana na waziri wa mambo ya nje wa Congo Marie Ntumba ambaye amesema wachunguzi tayari wanachunguza kisa hicho. 


"Serikali imeharikisha kuunda Tume siku ya Alhamis kufanya uchunguzi ili kubaini mazingira ambayo yalisababisha shambulio kwa msafara uliomjumuisha Balozi Attanasio na washirika wake. Serikali ya DRC inasisitiza hamu yake ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na washirika wake wote wa Magharibi na wengineo, kinyume na matangazo yaliyoripotiwa na vyombo fulani vya habari." Amesema Ntumba.

Lakini sasa wengine wanahoji kwamba uchunguzi haupaswi kuitishwa kwa mauaji ya balozi wa Italia pekee, bali wachunguzi wanapaswa pia kuweka kwenye ajenda yao, hali ya mauaji ya kila leo huko Beni na Ituri. Ndivyo wanavyodai baadhi ya wabunge wateuliwa wa Beni, mmoja wao ni Paul Muhindo Vawamawa:

Vyombo vya habari vya Congo vimeripoti balozi Luca Attanasio aliuawa na risasi ya jeshi la Kongo.
Vyombo vya habari vya Congo vimeripoti balozi Luca Attanasio aliuawa na risasi ya jeshi la Kongo. Picha: Justin Kabumba/AP/dpa/picture alliance

Soma pia:

"Kitu pekee kinachoombwa na Beni, kinachoombwa na Kivu Kaskazini pia Ituri, ni amani. Ninaamini kuwa wakati huu tunapowasaka wahalifu halisi wa kifo cha balozi, uchunguzi huo huo lazima pia uzingatiwe Beni ili wahalifu wa kweli wapatikane haraka." Amesema Muhindo.

Hata kabla ya mauaji ya Balozi huyo wa Italia, eneo la mashariki mwa Kongo limekuwa likikabiliwa mara kwa mara na mauaji yanayofanywa na makundi mbalimbali ya wahalifu na waasi dhidi ya raia, yakiwemo pia matukio ya ubakaji wanawake, utumikishaji watoto jeshini na utumwa wa kingono.

Kufuatia kuuawa kwa Balozi Luca Attanasio, mamlaka ya Kongo imeamua mwanadiplomasia yeyote yule atakayehitaji kufanya ziara katika maeneo ya mikoani, sharti aijulishe mapema serikali ili kusimamia usalama wake.