1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matumizi ya nguvu za kijeshi si suluhisho

P.Martin5 Januari 2009

Mapigano katika Ukanda wa Gaza na mpango wa pili wa msaada wa serikali ya Ujerumani kufufua uchumi ni miongoni mwa mada kuu zilizogonga vichwa vya habari katika magazeti ya Ujerumani leo Jumatatu.

https://p.dw.com/p/GSHo

Basi tutaanza na Mashariki ya Kati.Gazeti la MÜNCHNER MERKUR linasema:

Vitakuwa vita virefu na kuna kitisho cha kutokea umwagaji mkubwa wa damu.Israel haitoweza kushinda vita hivyo licha ya kuwa na nguvu kubwa za kijeshi.Vita hivyo vitachochea chuki mpya huku vikiimarisha misimamo mikali upande wa Waarabu na nchini Israel ambako uchaguzi wa bunge unafanywa tarehe 10 Februari.Kwa maoni ya MÜNCHNER MERKUR, katika historia hata mashambulizi mapya ya vikosi vya nchi kavu vya Israel katika Ukanda wa Gaza yatakumbusha kuwa mgogoro wa Mashariki ya Kati hauwezi kutenzuliwa kwa nguvu za kijeshi.

Gazeti la AUGSBURGER ALLGEMEINE likiendelea na mada hiyo hiyo linasema:

Moja ni wazi,Hamas haitosalimu amri.Raia wakizidi kuwa wahanga wa uvamizi,basi wafuasi wa itikadi kali ndio watazidi kuungwa mkono na umma uliohamasishwa sio katika nchi za Kiarabu na Kiislamu tu.Kwani mbele ya picha za watoto waliouawa,nani atakaeuliza masuala kujua yule wa kulaumiwa? Kiongozi gani wa Kiarabu atathubutu kuwalaani Hamas.

Kwa maoni ya gazeti la SÄCHSISCHE ZEITUNG ufunguo wa suluhisho la mgogoro wa Mashariki ya kati upo Teheran.Linaongezea:

Amani haitopatikana mradi Iran kwa msaada wa Hamas inataka kulifutilia mbali taifa la Israel kwenye ramani.Teheran na Washington zitakapokuwa na uhusiano usio na mivutano basi kutakuwepo uhusiano bora kati ya Waisraeli na Wapalestina vile vile.

Sasa tunapindukia mada inayohusika na mpango wa pili wa msaada wa serikali ya Ujerumani kufufua uchumi unaozorota.Gazeti la SÜDWEST PRESSE linasema:

Kutokana na somo lililopatikana ni busara kupunguza athari za uchumi unaodorora hata ikiwa serikali itakuwa na deni jingine.Lakini ukweli wa mambo usigubikwe na sauti zinazopazwa kuwa wapiga kura watanufaika. Kwani ukweli halisi ni kwamba,serikali ilisita sana kabla ya kukubali kuwapunguzia raia kodi ya mapato.Vile vile ni muhimu mno kufanywa marekebisho ya haraka katika mfumo wa malipo ya kodi,lakini marekebisho hayo yafanywe kwa uangalifu mkubwa na yasiwe propaganda ya uchaguzi ujao.

Tunamalizia kwa gazeti la NORDKURIER na mgogoro wa gesi kati ya Urusi na Ukraine.Linasema:

Mgogoro kati ya kampuni kubwa ya gesi ya Urusi Gazprom na nchi jirani Ukraine unazidi kusababisha wasiwasi katika nchi za Ulaya ya Magharibi. Kwani Kiev inaweza kulifunga bomba linalosafirisha gesi ya Urusi kupitia Ukraine.Hapo makaazi mengi katika Ulaya ya Magharibi yatakosa gesi ya kutia ujoto majumbani na mitambo ya nishati haitofanya kazi.Kwani hakuna chaguo mbadala.Kwa hivyo ulimwengu wa magharibi ukijikuta unatetemeka kwa baridi,hakuna wa kulaumiwa isipokuwa wao wenyewe.