Matumizi ya nguvu Tibet,magazetini Ujerumani | Magazetini | DW | 17.03.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Matumizi ya nguvu Tibet,magazetini Ujerumani

Suala kama michezo ya Olympic isusiwe linazusha mabishano miongoni mwa wahariri

default

Wakimbizi wa Tibet


Mada ziko nyingi magazetini hii leo,kuanzia ziara ya kansela wa Ujerumani bibi Angela Merkel nchini Israel hadi kufikia uchaguzi wa Iran.Lakini kilichochambuliwa kwa mapana na marefu ni machafuko  ya Tibet na michezo ya olympic ya msimu wa kiangazi katika jamhuri ya umma wa China.


Viongozi wa kijeshi wa China walikua na kazi kubwa kuwazuwia waandamanaji wa Tibet,miezi michache tuu kabla ya michezo ya Olympic kuanza.Damu imemwagika.Kwamba wanaspoti wa dunia waisusie michezo hiyo,fikra hiyo inaangaliwa na wengi miongoni mwa wanasiasa wa Ujerumani kua si ya maana.Mabishano moto moto kuhusu fikra hiyo yameripuka magazetini.Gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU kwa mfano linahisi "Bado China inaweza kuitumia fursa iliyoko ya kusitisha umwagaji damu.Gazeti linaendelea kuandika:


"Kinyume na malalamiko ya umma nchini Myanmar,ambapo walimwengu walikodoa macho bila ya kusema chochote,safari hii walimwengu wana turufu za nguvu kuweza kuitia kishindo serikali ya mjini Beijing.Mojawapo ya turufu hizo ni michezo ya Olympic ya msimu wa kiangazi:jumuia ya kimataifa inabidi iweke wazi kabisa kwamba hatua za umwagaji damu kukomesha malalamiko huko Tibet zinaweza kupelekea kususiwa michezo hiyo ya Olympic.Sio tuu  hadhi ya Beijing itachujuka, bali pia imani ya walimwengu kwa jamhuri ya umma wa China itaingia hatarini.Mwaka 1989 serikali ya mjini Beijing ilituma vifaru na matinga tinga kuwatawanya wanafunzi waliokua wakiandamana  katika uwanja wa "amani ya mbiguni" mjini Beijing.Viongozi wa mjini Beijing hawatasamehewa tena  na walimwengu wakisababisha mauwaji mengine kama yale."


Gazeti la HANDELSBLATT la mjini Düsseldorf linaandika:


Licha ya mvutano wa Tibet,China inashikilia itaandaa michezo hiyo ya Olympic,inayoungwa mkono pia na Dalai Lama.Ndo kusema China iachiwe ifanye ikitakacho?Kuna uwezekano wa kuona uamuzi wa kuisusia michezo hiyo ukawashawishi wachina wajifungamanishe zaidi na serikali yao.Kwa namna hiyo serikali ya Beijing itakua na kazi rahisi kuonyesha kisa cha Tibet ni njama tuu iliyoandaliwa.Kwa upande mwengine lakini kitisho kama hicho kinatoa fursa ya kuibuka changa moto ya kisiasa.Changamoto kama hiyo haistahiki kupuuzwa.Kwasababu bado masuala ya haki za binaadam ni kidonda ndugu nchini China.Na michezo ya Olympik ni njia mojawapo ya kulazimisha haki za binaadam ziheshimiwe.


Mhariri wa gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG anajiuliza kama wengi wenzake wafanyavyo:


"Walimwengu waseme nini dhidi ya matumizi ya nguvu ya Beijing na mitindo yake ya kuifuja fikra yenye ya michezo ya Olympic?Hakuna anaependelea michezo hiyo isusiwa,kama alivyoshauri mcheza sinema wa kimarekani Richard Gere kutokana na matumizi ya nguvu yaliyopelekea damu kumwagika huko Tibet.Isingekua vizuri na si haki pia tukitilia maanani juhudi za wanaspoti waliojiandaa kwa muda wote, kwa lengo  la kunyakua medali mjini Beijing.Kususiwa michezo hiyo ingemaanisha pia kuachana  moja kwa moja na fikra ya maana iliyoko nyuma ya michezo ya Olympic..


Gazeti la STUTTGARTER ZEITUNG linahisi


China itakua na kazi kubwa kuutanabahishia ulimwengu ,amani ndio malengo inayoyafuata.Wenye kuienzi nchi hiyo na wananchi wake wamelazimika kufumba mdomo kwa aibu na fadhaa.Lakini ikilazimika hata na firauni watu lazma wazungumze nae-kama alivyowahi kusema wakati mmoja Willy Brand,alipokua akijadiliana pamoja na  viongozi wa Urusi waraka wa ushirikiano pamoja na nchi za mashariki.Ndivyo hivyo inavyotakiwa.Tukiisusia michezo ya Olympic,China itazidi kujifungia badala ya kuacha milango wazi.


 • Tarehe 17.03.2008
 • Mwandishi Winkelmann, Gerd
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DPne
 • Tarehe 17.03.2008
 • Mwandishi Winkelmann, Gerd
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DPne
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com