Matumaini ya mazungumzo ya amani Mashariki ya Kati yafifia | Matukio ya Kisiasa | DW | 11.03.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Matumaini ya mazungumzo ya amani Mashariki ya Kati yafifia

Israel yasema ilikuwa kosa kutangaza ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi

Makamu rais wa Marekani Joe Biden (kushoto) na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu

Makamu rais wa Marekani Joe Biden (kushoto) na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu

Matumaini ya kufanywa majadiliano ya amani yasio ya moja kwa moja yanafifia, baada ya Wapalestina kusema kuwa hawatoshiriki katika majadiliano hayo mpaka Israel itakapobatilisha mipango ya kujenga nyumba 1,600 mpya za walowezi wa Kiyahudi katika Jerusalem ya Mashariki. Maelezo zaidi anayo Prema Martin.

Wapalestina wametamka hayo baada ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu hapo awali kuamua hivyo hivyo. Wakati huo huo Israel inazidi kushinikizwa na jumuiya ya kimataifa kuhusu mradi wa ujenzi wa makaazi ya Wayahudi uliotangazwa wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani Joe Biden katika Mashariki ya Kati, katika jitahada ya kufufua majadiliano ya amani kati ya Israel na Wapalestina. Biden alisema:

"Ni muhimu kwa pande zote mbili kuhakikisha kuwa kuna mazingira yatakayosaidia majadiliano kufanyika na sio kukorofisha."

Israel ikizidi kushinikizwa na jumuiya ya kimataifa, hii leo imesema ilikuwa kosa kutangaza mpango wa kujenga nyumba 1,600 katika Jerusalem ya Mashariki wakati wa ziara ya Biden. Afisa wa ngazi ya juu amesema, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alikuwa na mazungumzo marefu pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani Eli Yishai kuhusu tangazo hilo.

Biden alitarajia kuwa ziara yake ingesaidia kuzidisha uwezekano wa kufanywa majadiliano yasio ya moja kwa moja. Badala yake,amejikuta akishughulika na mvutano mpya uliosababishwa na tangazo la Israel.

Hiyo jana Biden mara nyingine tena alieleza fikra zake waziwazi alipozungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari pamoja na Rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas,katika mji wa Ramallah ulio katika Ukingo wa Magharibi.

Abbas / Palästinenserpräsident / Ramallah

Kiongozi wa Wapalestina Mahmoud Abbas

Nae Rais Abbas alisema, tangazo hili la Israel pamoja na uamuzi uliopitishwa hapo awali kujenga nyumba 112 kwa ajili ya walowezi wa Kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi, unadhoofisha imani na ni pigo kubwa kwa jitihada zilizofanywa miezi iliyopita kuanzisha majadiliano yasiyo ya moja kwa moja. Amesema, haitoshi kulaani tu mpango huo wa Israel bali unapaswa kuzuiliwa. Wapalestina wanaiangalia Jerusalem ya Mashariki kama mji mkuu wa taifa la siku za mbele la Palestina.

Wakati huo huo Umoja wa Ulaya imelaani uamuzi wa Israel. Katika taarifa iliyotolewa na mkuu wa sera za nje za Umoja wa Ulaya Catherine Ashton amesema, Umoja wa Ulaya unasisitiza kuwa kuambatana na sheria ya kimataifa, makaazi hayo si halali. Hata nchi moja moja za Umoja wa Ulaya zimeshambulia msimamo wa Israel. Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Milliband amesema huo ni uamuzi mbaya uliopitishwa wakati usio muwafaka. Uamuzi huo, amesema, utawapa nguvu wale wanaoshikilia kuwa Israel haitii maanani suala la amani.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imeeleza waziwazi kuwa tangazo la Israel halitopuuzwa. Mjumbe maalum wa Marekani katika Mashariki ya Kati, George Mitchell atalishughulikia suala hilo atakaporejea katika kanda hiyo wiki ijayo. Siku ya Jumatatu Mitchell alifanikiwa kupata makubaliano ya kuanzishwa majadiliano yasiyo ya moja kwa moja. Duru ya mwisho ya mazungumzo ya ana kwa ana yalivunjika Desemba mwaka 2008 kufuatia mashambulio yaliyofanywa na Israel katika Ukanda wa Gaza unaodhibitiwa na Hamas.

Muandishi: Martin,Prema/DPA/AFPE

Mhariri: Josephat Charo

 • Tarehe 11.03.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/MQPY
 • Tarehe 11.03.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/MQPY
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com