1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matumaini ya kumalizika vita Yemen yachomoza

Oumilkheir Hamidou
27 Novemba 2019

Ushirika wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia unapanga kuwaachilia huru waasi 200 wa Yemen na kuruhusu safari za ndege kuanza upya kutoka mji mkuu Sanaa. Uamuzi huo unaashiria uwezekano wa kumalizika vita nchini Yemen.

https://p.dw.com/p/3To2Q
Saudi-Arabien Riad | Einigung auf Friedensplan im Jemen
Picha: Reuters/Saudi Press Agency

Uamuzi huo unasadifu wakati ambapo mashambulio ya waasi wa Houthi dhidi ya Saudi Arabia  yamepungua na umepitishwa baada ya afisa wa ngazi ya juu mjini Riyadh kusema mwezi huu kwamba "ujia umefunguliwa" pamoja na waasi wanaoshirikiana na Iran.

Wagonjwa wanaohitaji matibabu wataruhusiwa kusafiri kutoka uwanja wa ndege wa Sanaa ambao ulikuwa umefungwa kwa shughuli za kibiashara tangu mwaka 2016-msemaji wa ushirika wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia, Turki al-Maliki amesema katika taarifa iliyochapishwa na shirika rasmi la habari la Saudi Arabia.

Ushirika huo umeamua "kuwaachia huru wafungwa 200", wanamgambo wa Houthi" na utarahisisha safari za ndege kutoka Sanaa,"kwa watu wanaohitaji matibabu", kwa ushirikiano pamoja na shirika la afya la kimataifa WHO-taarifa hiyo imeongeza kusema.

Wafungwa walipoachiwa huru na wahouthi kutoka jela moja ya mjini Sanaa
Wafungwa walipoachiwa huru na wahouthi kutoka jela moja ya mjini SanaaPicha: Reuters/K. Abdullah

Wahouthi wajiandaa kuwapokea waasi watakaoachiwa huru

Uamuzi huo umepokelewa vyema na wa Houthi huku kiongozi mkuu Mohammed Ali al Houthi akitoa wito wa kuandaliwa sherehe kubwa kuwakaribisha waasi watakaoachiwa huru."Tunaukaribisha uamuzi huo na kuwatolea wito pia wasitishe mateso na visa vya ukandamizaji hadi wafungwa wote watakapoachiwa huru" amesema al Houthi ambae ni kiongozi mkuu wa tawi la kisiasa la waasi, kupitia mtandao wa Twitter.

Ishara nyengine inayozusha matumaini, afisa wa ngazi ya juu wa serikali ya Saudi Arabia amesema  nchi yake imefungua "ujia ulio wazi" pamoja na waasi wa Houthi."Hatuwafungii milango yetu wahouthi" afisa huyo ambae hakutaka jina lake litajwe amewaambia maripota mjini Riyadh.

Uamuzi uliopitishwa jumanne ni ushahidi tosha kwamba mazungumzo kati ya wawakilishi wa Saudi Arabia na wale wa Houthi yanaanza kuleta tija" anasema msomi wa taasisi ya mataifa ya Ghuba, mjini Washington, Hussein Ibish.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri: Josephat Charo