Matumaini ya kufufua mchakato wa amani | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.07.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Matumaini ya kufufua mchakato wa amani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier anaamini kuwa majadiliano ya amani ya Mashariki ya Kati, kumaliza mgogoro kati ya Israel na Wapalestina yatafufuliwa upya.

Israeli President Shimon Peres, right, and German Foreign Minister Frank-Walter Steinmeier meet at the president's residence in Jerusalem, Monday, July 6, 2009. Steinmeier is on a Middle East trip that includes Israel, the Palestinian Territories, Syria and Lebanon. (AP Photo/Jonathan Nackstrand)

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier(kushoto) alipokutana na Rais wa Israel Shimon Peres mjini Jerusalem,Julai 6,2009.

Kwa maoni yake mchakato huo wa amani umepata msukumo baada ya kuungwa mkono upya na serikali ya Rais wa Marekani Barack Obama. Waziri Steinmeier alipoanza ziara yake ya siku mbili leo hii katika Mashariki ya Kati alisema, kuna matumaini ya kuona mwanzo mpya katika jitahada za kutafuta suluhisho la amani kati ya Israel na Wapalestina. Matumaini hayo yameibuka baada ya Rais Obama kutoa mwito si kwa Israel na Wapalestina tu, bali hata nchi jirani za Kiarabu kuunga mkono suluhisho la madola mawili.

Kabla ya kukutana na Rais wa Israel Shimon Peres,waziri huyo wa Ujerumani alisema, nchi za Kiarabu zenye siasa za wastani zijumuishwe katika mchakato wa Mashariki ya Kati. Baadae akasisitiza umuhimu wa kuanzisha upya majadiliano ya amani kati ya Israel na Wapalestina. Alisema:

" Njia pekee ya kuleta utulivu katika kanda nzima ni kujadiliana na Wapalestina."

Kwa maoni yake suluhisho la kuwa na madola mawili yaani Israel na Palestina ni suluhisho litakalohakikisha utulivu katika kanda hiyo. Suluhisho hilo hapo awali, lilipingwa wazi wazi na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu lakini mwezi uliopita, baada ya kushinikizwa na Marekani na viongozi wa Ulaya, aliashiria kuwa anataka amani na yupo tayari kujadiliana upya na Wapalestina. Lakini amekataa kusitisha kabisa ujenzi wa makazi ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi, sharti la Wapalestina la kurejea katika majadiliano ya amani.

Steinmeier amekiri kuwa suala la makazi ya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi iliyokaliwa na Israel kwenye Ukingo wa Magharibi ni sehemu ngumu kabisa ya majadiliano.Lakini hakuna njia ya kujiepusha na suala hilo kwani majadiliano ya kumaliza mgogoro wa Mashariki ya Kati hayatosonga mbele bila ya kuwepo mageuzi katika sera ya ujenzi wa makazi ya walowezi wa Kiyahudi.

Waziri Steinmeier wakati wa ziara yake mjin Jerusalem amekutana pia na mpatanishi mkuu wa Wapalestina katika mchakato wa amani, Saeb Erakat.Hapo awali alipanga kuonana na Rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas lakini mkutano huo ulifutwa kwa sababu ya ziara ya ghafla ya Abbas nchini Jordan. Kesho Jumanne, Steinmeier atakuwa na mazungumzo nchini Syria pamoja na waziri mwenzake Walid al-Muallem na Rais Bashar al-Assad mjini Damascus kabla ya kuelekea Beirut kukutana na Rais wa Lebanon Michel Sleiman na waziri mkuu mteule Saad Hariri.

Mwandishi: P.Martin/AFPE

Mhariri: M.Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com