1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matokeo ya muda ya kura ya maoni yatatangazwa kesho, Zanzibar

31 Julai 2010

Kura hiyo ya maoni inaazimia kumaliza uhasama kati ya CCM na CUF

https://p.dw.com/p/OZ3Y
Kisiwa cha Zanzibar kina raia laki nne waliojiandikisha kupiga kura.Picha: DW /Maya Dreyer

Kura ya maoni nchini Zanzibar imepigwa leo yenye lengo la kuamua ikiwa itakuwa na serikali ya umoja wa kitaifa baada ya uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba ili kusitisha uhasama uliokita mizizi na kuvuruga maendeleo katika kisiwa hicho cha Tanzania kwa miongo kadhaa.

Wapiga kura laki nne waliojiandikisha walishiriki katika Uchaguzi huo unaonuia kupitisha pendekezo la kufanywa marekebisho katika katiba yatakayotenga nyadhifa mbili za makamu wa rais zitakazogawanywa kati ya vyama vitakavyoshika nafasi ya kwanza na ya pili katika uchaguzi wa wawakilishi.

Uhasama kati ya chama kikuu cha CCM na CUF katika kisiwa hicho cha watu milioni 1.2, umekuwa ukikithiri na wakati mwingine kusababisha umwagaji damu tangu kuanzishwa kwa sera ya vyama vingi mwaka wa 1992.

Tume ya uchaguzi katika kisiwa hicho inatarajiwa kutangaza matokeo ya muda hapo kesho.

Mwandishi, Peter Moss/ AFP

Mhariri, Mohamed Dahman