1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matokeo rasmi ya uchaguzi Uganda kutangazwa jioni

Grace Kabogo
16 Januari 2021

Tume ya Uchaguzi nchini Uganda inaendelea kutangaza matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Januari 14, huku matokeo rasmi ya uchaguzi wa urais yakitarajiwa kutolewa Jumamosi jioni.

https://p.dw.com/p/3o08P
Bildkombo | Yoweri Museveni und Bobi Wine

Kwa mujibu wa matokeo yaliyotolewa usiku wa kuamkia Jumamosi, rais aliyeko madarakani, Yoweri Museveni anayewania nafasi hiyo kwa muhula wa sita kupitia chama tawala cha NRM anaongoza kwa asilimia 61.98, ambazo ni sawa na kura 4,340,134.

Mpinzani wa mkuu wa Museveni, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine mgombea wa urais kwa tiketi ya chama cha NUP amepata asilimia 30.91 ambazo ni kura 2,164,347.

Wagombea wengine hawajafikisha asilimia 5

Nafasi ya tatu inashikiliwa na mgombea wa chama cha Forum for Democratic Change, FDC, Amuriut Oboi Patrick ambaye kapata asilimia 3.64, ambazo ni sawa na kura 254,628 ya kura zilizohesabiwa.

Wagombea wengine wa urais hawajafikisha hata asilimia tano ya kura ambazo tayari zimehesabiwa. Hata hivyo, matokeo ya ngome kuu za Bobi Wine maeneo ya mji mkuu, Kampala pamoja na wilaya jirani bado hayajatangazwa.

Uganda | Opposition | Bobi WIne
Mpinzani Mkuu wa Museveni, Robert KyagulanyiPicha: Abubaker Lubowa/REUTERS

Matokeo hayo yanatangazwa wakati ambapo bado makaazi ya Wine yamezingirwa na askari wa usalama wakisema kuwa wanalinda usalama wake. Naibu Msemaji wa jeshi la Uganda, Deo Akiiki amesema wataendelea kuyalinda maakazi hayo, lakini hawana nia yoyote ya kumkataka kiongozi huyo wa upinzani kama inavyodaiwa. Lakini askari hao haijajulikana wataondoka lini.

Bobi Wine ameendelea kushikilia msimamo wake kuyapinga matokeo hayo akisema ni ya uongo. Wine amesema Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Uganda, Simon Byabakama alizipuuza kasoro zilizojitokeza wakati wa uchaguzi, vikiwemo vitendo vilivyofanywa na vikosi vya jeshi.

 

Bobi Wine ayapinga matokeo ya uchaguzi

Kwa upande wa matokeo ya uchaguzi wa wabunge, baadhi ya mawaziri wametupwa nje katika kinyang'anyiro hicho baada ya kushindwa kuvitetea viti vyao. Mawaziri walioshindwa ni pamoja na wa Biashara, Amelia Kyambadde na Waziri wa Kilimo, Vincent Sempijja.

Katika hatua ya kushangaza, Waziri wa Habari na Mwongozo wa Kitaifa, Judith Nabakooba ameshindwa kutetea kiti chake baada ya jimbo lake kunyakuliwa na mwandishi wa habari Joyce Bagala.

Ama kwa upande mwingine huduma ya mtandao wa intaneti bado haijarejea hadi sasa. Pia huduma za kutuma na kupokea pesa kwenye mitandao ya simu za mkononi nazo zimefungwa, hatua inayosababisha hali kuwa ngumu zaidi katika wakati huu.