1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matokeo rasmi ya uchaguzi Msumbiji

Mohamed Dahman12 Novemba 2009

Guebuza atangazwa rasmi mshindi wa uchaguzi wa rais Msumbiji

https://p.dw.com/p/KVTy
Rais Guebuza wa Msumbiji akipiga kura katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2009.Picha: picture alliance/landov

Rais wa Msumbiji aliekuwa akitetea kiti chake Armando Guebuza amepata ushindi mkubwa wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2009 nchini Msumbiji kwa kuzoa robo tatu ya kura.Matokeo hayo rasmi ya uchaguzi wa Msumbiji uliofanyika tarehe 28 mwezi wa Oktoba yametolewa leo hii na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo imetangaza kwamba Guebuza wa chama cha Frelimo amechaguliwa tena kwa kipindi cha miaka mitano baada ya kujisombea asilimia 75.4 ya kura.

Kiongozi wa upinzani wa muda mrefu wa chama cha Renamo Afonso Dhlakama amejipatia asilimia 16.5 ya kura asilimia 8.65 ya kura imekwenda kwa Davis Simango kiongozi wa chama kipya cha Mozambique for Demokratic Movement (MDM)chama cha Vuguvugu la Demokrasia nchini Msumbiji.

Chama tawala cha Frelimo kimejipatia ushindi mkubwa kwa kuzoa viti 191 kati ya viti 250 bungeni.Chama kikuu cha upinzani Renamo kimepata viti 51 na chama kipya cha MDM kilichoundwa baada ya kujiengua kutoka Renamo kimepata viti vinane.

Kabla ya uchaguzi huo Frelimo ilikuwa ina viti 190 na Renamo ilikuwa ina viti 60. Chama cha Frelimo kimekuwa madarakani kwa takriban miaka 34 tokea uhuru wa nchi hiyo kutoka Ureno hapo mwaka 1975.

Frelimo ina theluthi mbili ya wingi wa viti unaohitajika bungeni ili kuweza kubadili katiba ya nchi hiyo.Jambo hilo linampa Guebuza nafasi ya kubadili katiba kumruhusu kugombania urais kwa kipindi cha tatu madarakani.Katiba ya Msumbiji inaruhusu vipindi viwili tu madarakani kwa urais.

Hata hivyo wanachama waandamizi wa Frelimo wameweka wazi kwamba Guebuza hatogombania katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2014.Veronica Macamo afisa wa uchaguzi wa chama cha Frelimo amesema wingi wa viti walionao bungeni utawapa huru zaidi wa kuchaguwa kipi kilicho bora kwa wananchi wa Msumbiji. Amesema Frelimo imekuwa ikifanya kazi kwa manufaa ya wananchi na hivyo ndivyo itakavyoendelea kufanya katika serikali mpya.

Hata hivyo vyama vya upinzani Renamo na MDM vimeutangaza uchaguzi huo wa tarehe 28 Oktoba kuwa wa udanganyifu na wameituhumu Frelimo wa kujaza kura za bandia.Chama cha MDM kiliwasilisha kwa vyombo vya habari orodha ya waangalizi wa uchaguzi juu ya ukiukaji wa taratibu za uchaguzi uliotokea wakati wa uchaguzi.Chama cha MDM kinadai kwamba baadhi ya wafanyakazi katika vituo kadhaa vya uchaguzi walifanya uhalifu wa uchaguzi.Chama hicho kimeonyesha ukanda wa video uliorekodiwa kwa kutumia simu ya mkono ukionyesha wafanyakazi wa uchaguzi wakizitia mkono kura katika kituo cha uchaguzi cha Beira.

Licha ya madai hayo Tume ya Uchaguzi ya Taifa (CNE) imesema hakuna malalamiko rasmi yaliowasilishwa kwao juu ya ukiukaji wa taratibu za uchaguzi.

Vyama vya kisiasa vina siku mbili baada ya siku ya kupiga kura kuwasilisha malalamiko au ushahidi wa kukiukwa kwa taratibu za uchaguzi.Hatukupokea malalamiko yoyote yale katika kipindi hiki amesema hayo Leopoldo da Costa mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa nchini Msumbiji.

Zaidi ya waangalizi wa uchaguzi 1,000 wa kitaifa na kimataifa kutoka Umoja wa Afrika,Umoja wa Ulaya,Jumuiya ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADCC na Jumuiya ya Nchi Zinazozungumza Kireno zimeutangaza uchaguzi huo wa Msumbiji kuwa ni huru na wa haki.

Mwandishi :Mohamed Dahman /IPS

Mhariri:Abdul-Rahman