Mateka wanne wa Kichina wauwawa Sudan | Matukio ya Kisiasa | DW | 28.10.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mateka wanne wa Kichina wauwawa Sudan

Wafanyakazi wanne wa mafuta wa China miongoni mwa kundi la wafanyakazi tisa wa Kichina waliotekwa nyara nchini Sudan wameuwawa katika jaribio la kuwaokowa lililoshindwa.

Rais Hu Jintao wa China akikutana na Rais Omar al-Bashir mjini Beijing mwaka 2006.China inasema uwekezaji wake umekuwa ukiwanufaisha watu wa Sudan.

Rais Hu Jintao wa China akikutana na Rais Omar al-Bashir mjini Beijing mwaka 2006.China inasema uwekezaji wake umekuwa ukiwanufaisha watu wa Sudan.

Hayo yametaarifiwa leo hii na serikali ya China ambayo imesema itaendelea kuwekeza nchini humo licha ya kutokea kwa mauaji hayo na kwa upande wa serikali ya Sudan imeahidi kuimarisha uslama kwa wafanyakazi wa kigeni.

Mazingira kuhusiana na mauaji hayo yaliotokea hapo jana yamekuwa ya kutatanisha wakati kundi la waasi wa Dafur likikanusha madai ya Sudan kwamba lilikuwa linahusika na China ikibadili idadi ya vifo kutoka watano kuwa wanne.

Serikali ya Sudan awali ilisema kwamba wafanyakazi watano wa mafuta wa Kichina kati ya tisa waliotekwa nyara tarehe 18 mwezi wa Oktoba wameuwawa kwa kupigwa risasi na watekaji wao hapo jana na wawili walinusurika kwa kukimbia wakiwa na majeraha kidogo na wengine wawili wamendelea kushikiliwa mateka.

Leo wizara ya mambo ya nje ya China imesema wafanyakazi wake wanne wa mafuta wameuwawa .wanne wameokolewa na mmoja bado hajulikani alipo.

Sudan imekanusha kuwepo kwa mapambano yoyote yale kati ya vikosi vyake vya usalama na na watekaji nyara hao ikisisitiza kwamba ilikuwa tu ikishinikiza kuachiliwa kwao na njia za amani.

Lakini kiongozi mmoja wa kienyeji katika jimbo lenye mzozo la Kordofan Kusini ambapo Wachina hao walitekwa nyara na kuuwawa amesema Wachina hao wamekufa kutokana na mapigano kati ya jeshi la Sudan na wateka nyara wao.

Mtu mwengine katika eneo hilo ameliambia shirika la habari la AFP kwamba amewaona maafisa wa serikali ya Sudan wakikabidhi maiti tatu kwa balozi wa China huko Heglig ,wenzao wawili waliojeruhiwa na mmoja aliyeokolewa. Amedai kwamba wengine watatu hawajulikani walipo.

Maafisa waandamizi katika serikali ya Sudan hawakuweza kupatikana mara moja kuzungumzia tukio hilo.

Serikali ya China imeelezea fadhaa kubwa na kulaani kitendo hicho kitendo hicho kuwa cha kinyama na kigaidi kuuwa wafanyakazi wasiokuwa na silaha.Hata hivyo msemaji wa wizara hiyo amesema katika kipindi cha usoni China itaendelea kuthamini na kutekeleza sera ya urafiki kwa Sudan.

Wahandisi watatu na wafanyakazi wengine sita kutoka Shirika la Petroli la Taifa la China walikuwa wakifanya kazi kwenye eneo la mafuta la jimbo la Kordofan Kusini ambalo liko kwenye safu ya mzozo kati ya waliokuwa mahasimu hapo zamani Sudan kaskazini na kusini.

Duru za kidiplomasia zinasema Wachina hao tisa walitekwa nyara na makabila ya Waarabu lakini serikali ya Sudan inalilaumu kundi la waasi lenye nguvu kubwa huko Dafur la Vuguvugu la Haki na Usawa JEM kwa kuhusika na utekaji nyara huo.

Sudan imeahidi kuiamarisha usalama kwa shughuli za mafuta ambao ndio uhai wa uchumi wa nchi hiyo ulionawirisha mji mkuu wa Khartoum licha ya kuwepo kwa tafauti kubwa ya maendeleo nchini kote ambao mamilioni ya watu bado wanaishi kwenye dimbwi la umaskini.

Wakikanusha kuhusika na mauaji hayo waasi wa kundi la JEM ambalo serikali ya Sudana inasema ni la kigaidi wanasema wana vikosi katika eneo hilo na wanaungwa mkono na watu wa hapo na baadhi ya watu hao wa kabila la Messeria wamo katika kundi lao huenda wakachukuwa hatua lakini sio kwa kutumia jina la kundi la JEM.

Waasi wa Dafur wamekuwa wakiwateka nyara wafanyakazi wa mafuta mara nyingi wakilenga kampuni za Kichina kutokana na uhusiani wao mkubwa na serikali ya Sudan juu ya kwamba wote hunusurika bila ya madhara.

 • Tarehe 28.10.2008
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Fj6c
 • Tarehe 28.10.2008
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Fj6c
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com