Matarajio ya mkutano wa mjini Jeddah juu ya mafuta hayakutimia | Masuala ya Jamii | DW | 23.06.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Matarajio ya mkutano wa mjini Jeddah juu ya mafuta hayakutimia

Nchi ya Saudi Arabia, iliahidi katika mkutano wa mjini Jeddah kupandisha kiwango chake cha uzarishaji lakini matarajio ya kushusha bei ya mafuta hayakutimia

Wajumbe mkutanoni Jeddah

Wajumbe mkutanoni Jeddah

Katika mkutano huo wa siku mbili wa mjini Jeddah uliohitimishwa hapo jana, Saudi Arabia ilithibitisha kuwa kwa sasa hivi itatekeleza ahadi yake ya kuongeza mapipa laki mbili kwa siku kwa kiwango cha mafuta inayozarisha. Lakini hakuna mwafaka uliofikiwa juu ya sababu halisi zinazopelekea kupanda kupita kiasi bei ya bidhaa hiyo mahitajio muhimu. Wakati nchi zinazozarisha mafuta zinasisitiza ni makisio ya masoko, dola kupoteza thamani na misukosuko ya kisiasa katika maeneo kunakozarishwa mafuta kwa wingi ambavyo vimepelekea bei kupanda sana na wala sio upungufu, nchi za magharibi zilisitiza kuwa mahitajio ya mafuta yamepita uzarishaji.

Kwa maoni ya nchi hizo njia ya kulisuluhisha swala hilo la mafuta ni kuongeza uzarishaji kukidhi mahitajio. Waziri mkuu wa Uingereza alisema: "Sisi sote tunahitaji nia thabiti juu ya kuongeza mafuta na gesi. Kwa sababu hata kama tunapendekeza kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, mahitajio ya mafuta yatazidi kuwa makubwa kwa muda wa miaka michache ijayo“.

Mtaalamu katika maswala ya nishati John Hall amesema „ ikiwa wajumbe mkutanoni walikuwa wakitegemea kupata kitu cha maana kupunguza bei ya mafuta, hawakupa chochote“. Kulingana na mtaalamu huyo, vitisho vya Israel kuishambulia Iran na mashambulizi dhidi ya makampuni ya mafuta nchini Nigeria, vitapelekea bei ya mafuta kuzidi kupanda.

Leo asubuhi, bei imepanda kwa centi 76 kwa pipa ya mafuta yanayotarajiwa kuuzwa mwezi Agosti na kufikia dola 136,12 kwa pipa.

Saudi Arabia imekwenda mbali zaidi na kuahidi kuwa mnamo miaka ijayo itaweza kuongeza kiwango cha uzarsihaji na kufikia mapipa milioni 15 kwa siku ikihitajika. Hiyo ni habari njema kwamba mapipa milioni 2 na nusu zaidi zitapatikana kwenye masoko na kuyatuliza kiasi.

Hata hivyo, taarifa hiyo daima haitoshi. „Ingekuwa vizuri nchi nyingine zikaiga mfano huo wa Saudi Arabia“, amesema Fatih Birol, mkurugenzi wa sayansi katika Shirika la kimataifa la nishati. Kwani hakuna kitakachobadilika kwenye masoko kwa sasa hivi, wakati kiwango hicho cha milioni 15 za mapipa kitategemea hali itakavyokuwa miaka ijayo na wala sio sasa hivi.

Wataalamu wamezidi kusema japokuwa hakuna mwafaka uliofikiwa juu ya sababu zinazopelekea mafuta kuzidi kupanda bei, ang'alau mkutano huo wa mjini Jeddah uliweza kuwakusanya wanaozarisha na wanunuzi kubeba pamoja jukumu la mgogoro huo wa mafuta unaoikabili dunia.

 • Tarehe 23.06.2008
 • Mwandishi Nijimbere, Gregoire
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EOhQ
 • Tarehe 23.06.2008
 • Mwandishi Nijimbere, Gregoire
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EOhQ
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com