Matamshi ya Lieberman yamkasirisha Netanyahu na Wapalestina | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 29.09.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Matamshi ya Lieberman yamkasirisha Netanyahu na Wapalestina

Matamshi hayo ni kuhusu muda wa kupatikana kwa amani ya Mashariki ya Kati, ambapo amesema itachukua miongo kadhaa na siyo muda wa mwaka mmoja.

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Israel, Avigdor Lieberman.

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Israel, Avigdor Lieberman.

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Israel, Avigdor Lieberman amesema kuwa mkataba wa amani kati ya Israel na Wapalestina unaweza ukachuka miongo kadhaa. Matamshi hayo aliyoyatoa katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa yalimkasirisha kiongozi wake mwenyewe pamoja wa Wapalestina.

Akizungumza katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani, Bwana Lieberman alisema kuwa mzozo kati ya Israel na Palestina hautatizwi tu na masuala ya kivitendo, bali pia ya kihisia, kama vile kukosekana kwa uaminifu miongoni mwa pande hizo mbili, hivyo suluhisho la kupatikana kwa amani linaweza likachukua miongo kadhaa. Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu aliyakana matamshi hayo mara moja jambo linaloonyesha viongozi hao wawili kutofautiana kuhusu matarajio ya kupatikana kwa amani.

Matamshi hayo ya Waziri Lieberman yalipingwa na wajumbe wa Palestina na kusababisha waondoke katika kikao hicho. Mjumbe wa kudumu wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa, Riyad Mansour aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa matamshi hayo yalikuwa ya kukera na kwamba hakuna mtu anayeweza kuyavumilia. Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Bwana Netanyahu mjini Jerusalem imeeleza kuwa matamshi hayo hayakuratibiwa na waziri mkuu na kwamba Bwana Netanyahu ndiye anaongoza mazungumzo ya amani kwa upande wa taifa la Israel.

Taarifa hiyo ilifafanua kwamba masuala tofauti kuhusu makubaliano ya amani yatajadiliwa na kuamuliwa tu katika meza ya majadiliano na sio mahala pengine kokote. Bwana Lieberman ameyatoa matamshi hayo huku kukiwa na jitihada za wapatanishi wa amani kuisihi Israel irefushe muda wa kusimamisha kwa muda ujenzi wa makaazi ili kuyafanya mazungumzo hayo ya amani yaendelee, licha ya muda huo kumalizika siku ya Jumapili, hivyo kuiruhusu Israel kuendelea na ujenzi wa makaazi ya walowezi katika ardhi ya Wapalestina.

Hata hivyo, Bwana Netanyahu alikataa kurefusha muda huo wa kusitisha ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi. Mwanzoni mwa mwezi huu Bwana Netanyahu aliingia katika mazungumzo ya amani ya ana kwa ana yanayosimamiwa na Marekani kati yake na Rais wa Mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas kwa lengo la mkataba wa amani kufikiwa katika kipindi cha mwaka mmoja na hivyo kumaliza mzozo uliodumu kwa miaka 62 katika Mashariki ya Kati. Siku ya Jumatatu Rais Abbas aliondoa kitisho chake cha kujitoa kwenye mazungumzo hayo ya amani akisema kuwa uamuzi wake atautoa baada ya kushauriana na viongozi wa mataifa ya Kiarabu wiki ijayo mjini Cairo, Misri.

Waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Israel alisema Waisraeli sasa wanahitaji amani, lakini utata uliopo ni jinsi gani ya kupatikana kwa amani hiyo na namna ya kuwepo kwa hali ya usalama na utulivu katika eneo hilo. Amebainisha kuwa serikali ya muungano ya Israel sasa iko imara na katika suala la kupatikana amani inaungwa mkono na raia wengi nchini humo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE,DPAE)

Mhariri:Abdul-Rahman

 • Tarehe 29.09.2010
 • Mwandishi Kabogo, Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PPdy
 • Tarehe 29.09.2010
 • Mwandishi Kabogo, Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PPdy
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com