Matajiri wenye akaunti za siri nje | Matukio ya Kisiasa | DW | 05.04.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Matajiri wenye akaunti za siri nje

Nyaraka za siri kuhusu matajiri wakubwa wenye akaunti za siri nje ikiwemo familia ya rais wa Azerbaijan na aliyewahi kuwa mweka hazina wakati wa kampeni za uchaguzi za Rais wa Ufaransa, Francois Hollande, zimefichuliwa.

Waziri wa zamani wa bajeti wa Ufaransa, Jerome Cahuzac

Waziri wa zamani wa bajeti wa Ufaransa, Jerome Cahuzac

Gazeti la Ufaransa la Le Monde, limesema hatua ya kutajwa kwa Jean-Jacques Augier, ambaye aliwahi kuwa mweka hazina wakati wa kampeni za uchaguzi za Rais Francois Hollande, inaongeza shinikizo kwa Rais Hollande, ambaye tayari yuko katika wakati mgumu baada ya waziri wake wa zamani wa bajeti, Jerome Cahuzac, kufunguliwa mashtaka ya kukwepa kulipa kodi.

Nalo gazeti la Uingereza la The Gurdian limesema kuwa taarifa hizo zimetokana na nyaraka milioni mbili zilizofichuliwa pamoja na baruapepe zinazohusisha utajiri katika visiwa vya Uingereza vya Virgin na Cayman. Uchunguzi katika akaunti za siri za nje umefanywa na mashirika mbalimbali ya habari kwa kushirikiana na muungano wa waandishi wa habari wa kimataifa wanaoandika taarifa za upelelezi-ICIJ, wenye makao yake mjini Washington, Marekani.

Kwa mujibu wa gazeti la The Guardian, haimaanishi kuwa watu waliotajwa katika kashfa hiyo, wameweka fedha zao kwenye akaunti za nje kinyume na sheria, au kwamba jambo hilo ni la uhalifu, bali kitu pekee ni kwamba wametumia mamlaka waliyonayo kuwa na akaunti hizo kwa siri na hivyo kuwaruhusu kukwepa kulipa kodi.

Wanasiasa wakubwa watajwa

Mmoja wa wanasiasa mkubwa wa Mongolia, waziri wa zamani wa fedha, Bayartsogt Sangajav, ameiambia ICIJ kuwa alifikiria kujiuzulu baada ya ripoti kudai kuwa alikuwa na akaunti ya siri nchini Uswisi iliyokuwa na kiasi cha Euro 780,000.

Rais wa Azerbaijan, Ilham Aliyev

Rais wa Azerbaijan, Ilham Aliyev

Gazeti hilo linasema kuwa kampuni tatu zilianzishwa katika visiwa vya Uingereza vya Virgin mwaka 2008 zikiwa na majina ya watoto wa Rais wa Azerbaijan, Ilham Aliyev, ambao ni Arzu na Leyla. Katika orodha ya kampuni hizo, pia kuna jina la Hassan Gozal, tajiri mkubwa, ambaye kampuni yake imeshinda mikataba mikubwa nchini Azerbaijan, kama mkurugenzi.

Ama kwa upande mwingine, magazeti ya The Guardian na Le Monde yameripoti kuwa, Augier, ana hisa katika kampuni mbili zilizosajiliwa katika visiwa vya Cayman, ikiwemo nyingine iliyoko China. Hata hivyo, Augier ameliambia gazeti la Le Monde kuwa hajafanya jambo lolote kinyume na sheria na kwamba alikuwa anaunda ushirika na wajasiriamali wa kigeni.

Kashfa nyingine imemwangukia mke wa Igor Shuvalov, mfanyabiashara tajiri aliye karibu na Rais Vladmir Putin wa Urusi, ambaye aliwahi kuwa makamu wa kwanza wa waziri mkuu tangu mwaka 2008, ambaye rekodi yake inaonyesha kuwa ana akaunti kadhaa nje ya nchi. Aidha, wakili wa juu wa Canada na mume wa mbunge, Tony Merchant pamoja na Wacanada wengine 450 pia wametajwa katika ripoti hiyo iliyovuja. Tony alificha Cane milioni 1.7 za Canada katika visiwa cha Cook.

Msemaji wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Olivier Bailly, amesema umoja huo umezitaka nchi wanachama kulitafutia ufumbuzi suala la kukwepa kulipa kodi, akikadiria kuwa kiasi Euro trilioni moja zinafichwa kwa mwaka mmoja.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE
Mhariri: Josephat Charo

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com