1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa yanayoendelea yazidi kuvutana na mataifa yaliyoendelea katika mkutano Copenhagen

Sekione Kitojo15 Desemba 2009

Mkutano wa umoja wa mataifa wa hali ya hewa umeendelea na mkwamo leo Jumanne katika masuala muhimu, wakati rasmu mpya inakosa tarakimu kuhusu malengo ya kupunguza ongezeko la ujoto duniani.

https://p.dw.com/p/L3BQ
Waandamanaji wakiandamana mjini Copenhagen kuwashinikiza viongozi kupata makubaliano muhimu ya kupunguza utoaji wa gesi zinazoharibu mazingira.Picha: AP

Mkutano wa umoja wa mataifa wa hali ya hewa umeendelea na mkwamo leo Jumanne katika masuala muhimu, wakati rasimu mpya inakosa tarakimu kuhusu lengo la kupunguza ongezeko la ujoto duniani, wakati viongozi wa dunia wanajaribu kuongeza mbinyo ili yapatikane matokeo.

Wakati huo huo waziri wa mazingira wa India ameonya kuwa mazungumzo ya mjini Copenhagen bado yanakosa uwazi na huenda yakavunjika kuhusiana na masuala muhimu ambayo hayajatatuliwa ikiwa zimebaki siku tatu tu kabla ya kumalizika.

Mapendekezo mapya hayakutoa tarakimu katika lengo la muda mrefu la kupunguza gesi zinazoharibu mazingira, kiwango cha juu cha utoaji wa gesi hizo ,lengo linalotarajiwa la upunguzaji wa ongezeko la ujoto duniani , ama katika kutoa fedha kwa mataifa masikini ambayo yanaathirika na mabadiliko ya hali ya hewa.

Masuala haya ya msingi yanajadiliwa kwa makundi mbali mbali ya mawaziri wa mazingira, katika matumaini ya kupata muafaka ifikapo siku ya Ijumaa, wakati makubaliano yatakapowasilishwa kwa viongozi kutoka duniani kote. Wakati majadiliano hayo ya siku 12 tayari yakiwa yamegubikwa na mivutano ya kiutendaji na kunyosheana vidole, kuwasili kwa baadhi ya viongozi wenye uzito kunalenga katika kutia nguvu majadiliano.

Waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown , mwenzake wa Australia Kevin Rudd na rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva ni miongoni mwa wale wanaotarajiwa katika mji mkuu huo wa Denmark katika juhudi za kufikisha mwisho mkwamo huo.

Ban Ki-moon auf Kopenhagener Klimagipfel
Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-moon akizungumza na waandishi habari kabla ya kwenda Copenhagen kwa mkutano wa umoja wa mataifa wa hali ya hewa.Picha: AP

Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-moon amewasili mjini Copenhagen leo asubuhi baada ya kutoa onyo kuwa muda unakwenda mbio kuweza kupata makubaliano na kwamba kushindwa kutaleta hatari ya matokeo ya kiwango cha maafa.

Mkutano huo ambao unafikia kilele chake siku ya Ijumaa wakati viongozi 120 wa kitaifa na serikali watakapokutana mjini Copenhagen , unaonekana kuwa mkutano muhimu sana katika enzi ya baada ya vita vikuu vya pili vya dunia.

Lengo la mkutano huo ni kupata makubaliano juu ya mkataba ambapo mataifa yatatoa mapendekezo ya kupunguza utoaji wa gesi za carbon na kuweka mfumo wa kutoa mabilioni ya dola kuyasaidia mataifa masikini katika kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa. Iwapo ongezeko la utoaji wa gesi hizo halitazuiwa , sayari ya dunia itakuwa inaelekea katika muda wa muongo ujao katika ongezeko la ujoto ambalo litasababisha mafuriko, ukame, vimbunga na kupanda kwa viwango vya bahari kwa mamilioni ya watu , wanasema wanasayansi.

Lakini tofauti kubwa zinaendelea kuwapo juu ya kugawana majukumu. Mataifa yanayoendelea yanadai kuwa wenzao wa mataifa tajiri wapunguze utoaji wao wa gesi za carbon kwa takriban asilimia 40 ifikapo 2020 ikilinganishwa na viwango vya mwaka 1990. Waziri wa mazingira wa Ujerumani Norbert Röttgen amesema.

Katika mkutano huu kunakuwa na hali ya kutoaminiana kati ya nchi za viwanda na zinazoendelea na kuweka wazi, kwamba nchi zenye viwanda zionyeshe lengo lao la upunguzaji zaidi wa gesi zinazoharibu mazingira na kwamba sisi hatukimbii jukumu hilo. Na mkataba ambao unatakiwa na kila mmoja sio tu kwa yale mataifa yaliyoidhinisha mkataba wa sasa wa Kyoto lakini pia tunasisitiza umoja.

Mataifa yanayoinukia kiuchumi kama China na India yanasema kuwa yako tayari kuahidi hatua zao za kupunguza makadirio yao utoaji wa gesi hizo lakini yako katika mbinyo kutoa ahadi kubwa zaidi pia ziweze kuwekewa uchunguzi wa kimataifa.

Akijaribu kupunguza mvutano huo katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-moon amesema kuwa mataifa tajiri na masikini ziache kunyosheana vidole na ni lazima ziongeze mapendekezo yao ya kupunguza utoaji wa gesi zinazoharibu mazingira.

Pia nchi tajiri hazijatoa kwa mataifa yanayoendelea msaada wa kutosha ili kuweza kupatikana makubaliano juu ya kupambana na ongezeko la ujoto dunia. Amesema hayo rais wa halmashauri ya umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso wakati akijitayarisha kwenda katika mazungumzo hayo mjini Copenhagen.

Waziri wa mazingira wa India Jairam Ramesh amesema kuwa mazungumzo ya hali ya hewa mjini Copenhagen hayana uwazi na huenda yakavunjika kuhusiana na masuala muhimu. Jairam amesema kuwa kuna hali ya kukanganya na ukosefu wa uwazi katika wakati huu. Mazungumzo hayo yamekwama katika suala la nani anapaswa kupunguza gesi zinazosababisha kupanda kwa ujoto duniani, kwa kiasi gani na nani atalipa. Wakati muda unakwenda mbio , nafasi ya kupata mkataba utakaweza kuyabana mataifa kisheria inapotea lakini bado kuna matumaini ya kupata mkataba wa kisiasa zaidi .

Mwandishi:Sekione Kitojo / RTRE/ AFPE / DPAE

Mhariri:Abdul-Rahman