1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa yakutana kuijadili IS nchini Libya

16 Mei 2016

Mataifa kadhaa yenye nguvu duniani yanakutana leo katika mji mkuu wa Austria, Vienna kujadili kuongezeka kwa ushawishi wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS nchini Libya, ambako ni kitisho kwa Ulaya.

https://p.dw.com/p/1IoQf
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry (kulia) na mwenzake wa Urusi Segei Lavrov
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry (kulia) na mwenzake wa Urusi Segei LavrovPicha: Getty Images/AFP/J. Martin

Mkutano huo unaongozwa kwa pamoja na Marekani pamoja na Italia ambayo ni mkoloni wa zamani wa Libya, na ambayo imekuwa ikitaabika kutokana na idadi kubwa ya wahamiaji wanaoingia kwenye ardhi yake, wakitokea Afrika Kaskazini.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani John Kirby, amesema mkutano huo wa leo utatakafari msaada ya jumuiya ya kimataifa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya, kwa kuangazia zaidi masuala ya kiusalama.

Wenyekiti wa mkutano huo ni waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry, na mwenzake wa Italia Paolo Gentiloni. Gentiloni amesema kabla ya mkutano huo, kuwa nguvu za pamoja zinahitajika kusaidia mchakato wa kurejesha utulivu nchini Libya.

Uungwaji mkono nje, upinzani ndani

Serikali hiyo inayoongozwa na mfanyabiashara Fayez al-Sarraj inaungwa mkono kimataifa katika juhudi za kuiunganisha tena nchi, lakini inakabiliwa na upinzani wa ndani.

Serikali ya Umoja wa Kitaifa Libya inakabiliwa na upinzani mkubwa ndani ya nchi.
Serikali ya Umoja wa Kitaifa Libya inakabiliwa na upinzani mkubwa ndani ya nchi.Picha: picture alliance/dpa

Bado haiungwi mkono na bunge lililochaguliwa nchini humo, na mtu aliyetangaza kuwa mkuu wa majeshi Khalifa Haftar, mshirika wa bunge hilo ambaye ameapa kuyaangamiza makundi ya kiislamu nchini Libya.

Hata serikali kinzani yenye makao mjini Tripoli imekataa kuitambua serikali hiyo ya umoja wa kitaifa.

Katika mazingira hayo ya mgawanyiko, IS imejiimarisha katika eneo linalouzunguka mji wa Sirte kwenye ufukwe wa Mediterania, ambao imeugeuza kituo cha mafunzo kwa wanajihadi kutoka maeneo yote ya karibu na ya mbali.

Tumbo joto kwa Ulaya na Marekani

Ulaya ina wasiwasi kwamba wanajihadi hao ambao wamekuwa wakijikusanya upya, watautumia uwanja wa ndege wa Sirte na bandari ya mji huo, kuanzisha mashambulizi dhidi ya bara la Ulaya.

Wapiganaji wa IS wamejiimarisha katika mji wa Sirte
Wapiganaji wa IS wamejiimarisha katika mji wa SirtePicha: Getty Images/AFP/M.Turkia

Hivi karibuni ripoti ya bunge la Uingereza ilisema kuwa operesheni ya Umoja wa Ulaya baharini kupambana na magenge yanayosafirisha watu kimagendo imeshindwa.

Wasiwasi huo unakwenda sambamba na hofu ya Marekani, ambako maafisa wa serikali na wanadiplomasia wamesema ipo mipango ya kufikiria jinsi ya kuiondolea Libya vikwazo vya kuagiza silaha kutoka nje, ambavyo iliwekewa na Umoja wa Mataifa miaka mitano iliyopita.

Afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Marekani ameliambia shirika la habari la AFP, kwamba washirika wako tayari kuisaidia serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya, ikiwa itatoa maelezo ya kutosha na yenye kueleweka, juu ya namna inavyopanga kupambana na kundi la Dola la Kiislamu.

Maelezo hayo ndio yanayotarajiwa kuzungumziwa na Kerry na wenzake katika mkutano wa Vienna, lakini kuna mashaka ikiwa serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya itawasilisha mpango kamili wa kutaka usaidizi.

Nguvu zilizotawanywa

Mgawanyiko nchini Libya ulizidi makali hivi karibuni, pale pande mbili zinazopingana, serikali ya Umoja wa Kitaifa, na vikosi vinavyoongozwa na Khalifa Haftar, zilipotangaza mipango ya kupambana na IS, kila upande kivyake.

Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi katika baraza la seneti la Italia Nicola Latorre alisema hali hiyo ni kosa linalopaswa kuzuiliwa, na kuongeza kuwa hawataendelea kuukubali mgawanyiko huo.

Suala jingine litakalojadiliwa katika mkutano wa Vienna ni la wahamiaji haramu wanaoendelea kumiminika Ulaya, na mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini amesema atajadili uwezekano wa kurefusha operesheni ya kupambana wa wasafirishaji haramu wa watu hao.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe

Mhariri:Josephat Charo