Mataifa ya Ulaya kujadili suala la wakimbizi | Matukio ya Kisiasa | DW | 11.09.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mataifa ya Ulaya kujadili suala la wakimbizi

Mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani na Luxembourg wanatarajia kukutana na wenzao wa Jamuhuri ya Czech, Hungary, Poland na Slovakia mjini Prague kwa ajili ya kujadili suala la wakimbizi.

Rais wa Halimashauri ya umoja wa Ulaya Jean- Claude Junker

Rais wa Halimashauri ya umoja wa Ulaya Jean- Claude Junker

Mataifa ya ukanda huo yalikataa suala hilo la kugawana wakimbizi juma lililopita na kusema kuwa umoja wa ulaya ni lazima utafute chanzo cha mgogoro huoi kwanza ikiwa ni pamoja na kulinda mipaka inayounganisha mataifa hayo kwa kutumia mfumo huru wa hati ya kusafiria ndani ya mataifa yanayounda mkataba wa Shengen na pia kupambana na wafanyabiashara wasafirishaji wa wakikimbizi.

Hata hivyo Ujerumani ambayo iko msitari wa mbele hivi sasa katika kushughulikia suala hilo la wakimbizi imesema kuwa mpango uliowekwa na Rais wa halimashauri kuu ya ulaya Jean- Claude Junker wa kushughulikia suala hilo hautoshi peke yake kwa sasa kutatua tatizo hilo la wakimbizi ambalo ni kubwa zaidi tangu kumalizika kwa vita vikuu vya pili.

Wakimbizi wanaoingia nchini Hungary waongezeka.

Wakimbizi waliowasili nchini Hungary

Wakimbizi waliowasili nchini Hungary

Idadi ya wakimbizi wapatao 3,321 walioingia nchini Hungary hapo jana ni kubwa zaidi kuwahi kutokea ndani ya saa 24, na ilisababisha waratibu wa safari za treni nchini Austria kusimamisha huduma hiyo kwa muda kutokana na msongamano wa abiria katika treni hizo.

Wengi wa wakimbizi wanaharakisha kuvuka mpaka kuingia nchini Hungary kabla ya taifa hilo kuanza utekelezaji wa sheria ngumu dhidi ya wakimbizi ifikapo Septemba 15, hatua ambayo inaonekana kupingwa na shirika la umoja wa mataifa linaloshughulikia wakimbizi.

Inakadiriwa kuwa ifikapo juma lijalo kiasi cha wakimbizi 42,000 watakuwa wameingia nchini Hungary ili kuwahi kabla ya sheria hiyo kuanza kutumika.

Mataifa yanayounda umoja wa ulaya hadi sasa yamegawanyika katika msimamo kuhusiana na jinsi ya kushughulikia na kugawana mzigo huo wa wakimbizi.

Kulingana na utaratibu wa ugawanaji wa idadi ya wakimbizi uliotolewa wiki hii, Ujerumani itapaswa kuchukua zaidi ya wakimbizi 31,000, Ufaransa 24,000 na Uhispania wakimbizi 15,000 wakati Uingereza tayari imeahidi kuchukua wakimbizi 20,000 kutoka nchini Syria walioko katika makambi ya wakimbizi nje ya mataifa yanayounda umoja wa ulaya.

Wakati hayo yakiendelea wabunge wa mataifa ya umoja wa ulaya wamependekeza pia kuwepo kwa kongamano la kimataifa litakalojadili suala la wakimbizi likihusisha mataifa ya Marekani, Umoja wa mataifa na mataifa ya kiarabu.

Akijibu hoja ya kwanini Marekani imekua nyuma katika kusaidia mzigo huo wa wakimbizi, Rais Barack Obama aliahidi kupokea kiasi cha wakimbizi 10,000 wa Syria katika kipindi cha kuanzia Oktoba mosi mwaka huu.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani Josh Earnest amesema pia kuwa rais Obama ameagiza kuongeza idadi hiyo ya wakimbizi kutoka nchini Syria kutoka 1,500 baada ya wamarekani 62,000 kusaini waraka wa maombi wa kukubali taifa hilo kupokea wakimbizi zaidi.

Mwandishi : Isaac Gamba/AFPE/DW

Mhariri :Gakuba Daniel

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com