1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa ya magharibi yapongeza kukamatwa kwa Karadzic

Kalyango Siraj23 Julai 2008

Yeye asema atapinga kupelekwa The Hague

https://p.dw.com/p/EiHU
Radovan Karadzic kama alivyo kwa sasaPicha: AP

Mabalozi wa mataifa ya magharibi katika Umoja wa mataifa wameielezea hatua ya kukamatwa kwa kiongozi wa zamani wa WaSerbia wa Bosnia Radovan Karadzic kama alama inayotia moyo kwa mahakama ya makosa ya uhalifu wa kivita ya Umoja wa mataifa pamoja na Umoja wa Ulaya.

Karadzic mwenyewe anasema kuwa atapinga hatua ya kumpeleka The Hague.

Radovan Karadzic ambae alikamatwa mjini Belgrade akiwa amejifanya kama mshairi na Daktari,anatarajiwa kufikishwa katika mahakama ya uhalifu wa kivita ya mjini The Hague Uholanzi baada ya kukamilisha utaratibu unaohusika.

Hata hivyo yeye amesema atafanya juu chini kuona kama hapelekwi huko.

Amekuwa akitafutwa na mahakama hiyo tangu mwaka wa 1995 kutokana na maovu katika eneo la Bosnia.Kati ya mwaka 1992 hadi 1995 kulitokea vita katika eneo la Balkani na yeye kama kiongozi wa Waserbia wa Bosnia wa wakati huo akiwa pamoja na mshirika wake mkuu na kamanda wa jeshi lake wakati huo Ratko Mladic ambae baado amejificha anabeba dhamana ya mauaji hayo.

Mashtaka yanayomkabili ni kama vile mauji ya halaiki,mauaji, kukusudia kuua, kuwahamisha watu kwa nguvu na visa vya kinyama dhidi ya waislamu,waCroatia pamoja na raia wengine ambao hawakuwa Serbia wakati wa vita vya Bosnia.

Aidha shinikizo linatolewa kwa serikali ya Serbia la kumkamata haraka mshirika wake Generali Mladic.

Karadzic ambae siku ya leo jumatano amekaa korokoroni kwa siku ya pili ,serikali ya Serbia ilitaka kumhamisha kwa mahakama ya uhalifu wa kivita mapema iwezekanavyo ,lakini huenda isifanikiwe. Kisheria ana siku tatu za kukataa rufaa.Lakini wakili wake amesema kuwa atawasilisha maombi yake siku ya Ijumaa.

Mbali na hayo kukamatwa kwake kumepongezwa na mataifa ya magharibi.

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amekuita kukamatwa kwake kama tukio la kihistoria.

Yeye waziri wa mashauri ya kigeni wa Canada David Emerson katika taarifa alioitoa amenukuliwa kusema kuwa hatua hiyo itasaidia kuwaleta pamoja wale walioathirika na vita vibaya vya miaka ya 1990.

Nae Kamishna wa Umoja wa Ulaya anehusika na kupanuliwa kwa umoja huo Oli Rehn nae alikuwa na ujumbe huohuo.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Zalmay Khalilzad alisema kuwa Karadzic anabeba dhamana la uhalifu mbaya kuwahi kutendwa katika bara la Ulaya tangu vita vikuu vya pili vya dunia na kwa mantiki hiyo akaongeza kuwa wanafurahia kukamatwa kwake na kutaraji kuwa pia nae mwenzake Mladic atakamatwa.

Pia mwito wa kukamtwa kwa Mladic umetolewa na waziri wa mashauri ya kigeni wa Ufaransa Bernard Kouchner.