1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa ya mafuta Afrika yatahadharishwa

4 Desemba 2007

Wataalamu wanasema mipango mbadala haina budi kutiliwa maanani kwani kunasiku mafuta yatamalizika.

https://p.dw.com/p/CWkf

Mataifa yenye utajiri wa mafuata barani Afrika yametakiwa kujiepusha na ubathirifu wa mapato yao yanayotokana na bidhaa hiyo, iwapo wanataka kujilinda na janga pale visima vitakapokauka.

Tahadhari hiyo imetolewa katika mkutano wa wataalamu uliofanyika karibuni katika jiji la biashara la Johannesburg nchini Afrika kusini.

Mafuta mara nyingi yamekua ni bidhaa

adimu kwa Afrika, huku bara hilo kwa sehemu kubwa likitegemea makampuni ya kigeni na kwa upande mwengine kuendeshawa na viongozi awala rushwa hata miongoni mwa baadhi ya nchi zenye utajiri huo wa mafuta.

Wakati hali hiyo imeanza kubadilika panapohusika na jinsi wanavyosimamia utajiri huo, lakini wanahitaji kuwa na zingatio mbadala kabla ya visima havijakauka.

Diarmind O´Sullivan kutoka taasisi ya Global Witness yenye makao yake mjini London, aliuambia mkutano wa siku mbili mjini Johannesburg ulioandaliwa na taasisi ya masuala ya kimataifa ya Afrika kusini kwamba , mafuta ni utajiri unaofanana na pombe . Kama huna mhimili itakuyumbisha.

Bw O´ Sullivan alisema nchi kama Angola, ambayo sasa ni moja ya zinazokua haraka kiuchumi barani Afrika kutokana na utajiri wake wa mafuta, inaakiba ya karibu miaka 20, na kama hiyo itapotea kwa sababu ya rushwa na utawala mbaya, tija hiyo haiwezi kurudi tena. “Mafuta yakitoka yametoka.”

Wachambuzi katika mkutano huo walisema hali za kimaisha katika nchi nyingi zenye utajiri wa mafuta kwa kawaida ni mbaya zaidi kuliko za wale walioko katika nchi zisizobarikiwa na utajiri huo.

Kwa mujibu wa wachambuzi Angola ni muagizaji mkubwa wa magari ya kifahari kutoka n´gambo, licha ya kwamba kiasi ya asili mia 70 ya wakaazi wake wanapato la chini ya dola moja kwa siku. Taifa hilo la kusini mwa Afrika linatoa karibu mapipa milioni mbili ya mafuta kwa siku, na sasa ni moja wapo ya wasafirishaji mafuta wakubwa kuelekea China, ambayo ina vitega uchumi vikubwa nchini Angola ikiisaidia pia katika ujenzi wa miundo mbinu kama barabara na kadhalika, iliyoharibiwa kutokana na vita vya miaka 27 vya wenyewe kwa wenyewe miaka iliopita.

Bajeti ya Angola inakadiriwa kufikia dola 31 bilioni, wakati iadadi ya watoto wanaofariki kabla ya kutimia miaka mitano ni kubwa duniani hii leo.

Huko Guinea ya Ikweta ambako umoja wa mataifa unakadiria asili mia 80 ya pato lake imo mikononi mwa asili mia tano tu ya wakaazi, matumizi katika sekta ya huduma za kijamii kama afya na elimu yamepungua mno, licha ya kuongeza pato la linalotokana na mafuta.

Kwa mujibu wa mtaalamu Alex Vines ,Nigeria mtoaji mkubwa kabisa wa mafuta barani Afrika na ambayo imepiga hatua kubwa katika kuweka uwazi na kupambana na rushwa, imeshuhudia umasikini ukiongezeka kutoka asili mia 30 ya wakaazi katika mwaka wa 1970 hadi asili mia 70 mwaka 2000.

Kukiwa na mmiminiko mkubwa wa bidhaa kutoka nje, utawala bora na usimamizi mzuri wa mali asili ni mambo ambayo yangeweza kuifaidisha sana Afrika, lakini Bw Vines anaonya kwamba nchi zenye utajiri wa mafuta zinapaswa kuwa na mpango mbadala kuendeleza uchumi, kwani mafuta pekee hayawezi kuziondolea umasikini. Afrika alisema “ Sio Saudi Arabia.”

Mkutano huo mjini Johannesburg pia uliwasikiliza wajumbe wakizungumzia jinsi nchi chache sana zinavyosimamia mali nyengine za asili kama mbao na hata shughuli za uvuvi, ingawa Afrika kusini na Botswana zenye utajiri wa almasi zilitajwa kama mfano wa pekee.

Matumaini na wasi wasi kwa wakati mmoja ni jambo lililozungumzwa panapohusika na Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo, Sierra Leone na Liberia.

Hatimae ukatolewa wito kwa jamii ya kimataifa kutafakari mara mbili, kabla ya kuweka rasili mali zinazoimarisha tawala zinazokandamiza demokrasia na haki za binaadamu barani Afrika na wakati huo huo ikasisitizwa kwamba mashindano ya kuwania uwekezaji barani humo yanapaswa kutupiwa jicho.