1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa kujadili udhibiti wa biashara ya silaha

18 Machi 2013

Wawakilishi kutoka mataifa 150 wanakutana leo mjini New York Marekani, katika shinikizo la mwisho la kuunda mkataba wa kimataifa, unoalenga kukomesha uuzaji wa silaha kiholela, lakini Marekani inashinikizwa kuukataa.

https://p.dw.com/p/17zMH
Mzinga ya Korea Kaskazini.
Mzinga ya Korea Kaskazini.Picha: picture-alliance/dpa

Wanaharakati wa udhibiti wa silaha na watetezi wa haki za binaadamu wanasema mtu mmoja anakufa kila dakika duniani kote kutokana na vurugu zinazohusiana na silaha, na kwamba kunahitajika mkataba unaoyafunga mataifa kudhibiti uuzaji wa silaha kiholela, ambazo wanasema huchochea vita, ukatili na ukiukaji wa haki za binaadamu.

Biahsara ya silaha ina thamani ya dola za Marekani bilioni 70 kwa mwaka.
Biahsara ya silaha ina thamani ya dola za Marekani bilioni 70 kwa mwaka.Picha: AP

Mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa ulipiga kura mwezi Desemba kuanzisha tena majadilano wiki hii, juu ya kile kinachoweza kuwa mkataba wa kwanza wa kimataifa wa kudhibiti biashara ya silaha yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 70 - kuanzia meli za kivita, vifaru na helikopta za mashambulizi, hadi kwenye bunduki za kawaida. Hii ni baada ya mkutano wa awali uliofanyika mwezi Julai mwaka 2012, kuvunjika kwa sababu Marekani, na baadaye Urusi na China, zilitaka zipewe muda zaidi.

NRA yamshinikiza Obama aukatae

Wajumbe wa mkutano wa Julai walisema utawala mjini Washington ulitaka kusogeza suala hilo mbele ya uchaguzi wa rais uliyofanyika mwezi Novemba ingawa serikali ya Obama ilikanusha madai hayo. Majadiliano ya sasa yatakwenda hadi Machi 28. Marekani inasema inahitaji mkataba imara, lakini rais Obama yuko chini ya shinikizo kutoka kwa chama chenye nguvu cha wamiliki wa silaha nchini humo, NRA, kuzuia mkataba huo. Chama hicho kimeapa kuwa kitazuia kuridhiwa kwa mkataba huo ndani ya baraza la Seneti, kama utawala wa Obama utauunga mkono ndani ya Umoja wa Mataifa.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, John Kerry, alionyesha yuko tayari kuunga mkono mkataba huo kwa masharti siku ya Ijumaa, akisema Marekani bado inasimamia dhamira yake ya kupatiakana kwa mkataba imara na wenye ufanisi, utakaosaidia kushughulikia madhara makubwa ya biashara hii ya silaha kwa amani na utulivu wa dunia. Lakini alirudia kuwa Marekani, ambayo ndiyo nchi ya kwanza duniani kwa kutengeneza silaha, haitaukubali mkataba unaoingilia haki ya raia wa Marekani kumiliki silaha, jambo ambalo ni nyeti sana kisiasa nchini humo.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry amesema serikali yake itaunga mkono mkataba wa udhibiti wa silaha kwa masharti.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry amesema serikali yake itaunga mkono mkataba wa udhibiti wa silaha kwa masharti.Picha: Reuters

Lengo la mkataba

Lengo la mkataba huu ni kuweka viwango vya uhamishaji wa silaha zozote zinazovuka mipaka, ziwe nzito au nyepesi. Mkataba huo utaweka pia masharti kwa mataifa kuangalia upya mikataba ya silaha, kuhakikisha hazitumiki katika ukiukaji wa haki za binaadamu, kukiuka vikwazo vya kimataifa na hazibadilishwi matumizi kinyume na sheria.

Wanadiplomasia wanasema iwapo mkataba huo utashindwa kupata uungwaji mkono unaohitajika kwa sababu Marekani, Urusi au nchi nyingine inayotengeneza silaha kwa wingi inaupinga, mataifa yanaweza bado kuupigia kura ndani ya baraza la Umoja wa Mataifa. Chaguo lingine ni kuurekebisha mswada huo na kuufanya ukubalike na Marekani na wajumbe wengine.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre
Mhariri: Josephat Charo