1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa kadha yajaribu kuunusuru mkataba wa nyuklia na Iran

Amina Mjahid
22 Desemba 2020

Mataifa yaliobakia katika mkataba wa nyuklia wa Iran wa mwaka 2015, yamesema siku ya Jumatatu yanajitayarisha kuikaribisha tena Marekani katika mkataba huo chini ya utawala wa Joe Biden.

https://p.dw.com/p/3n2aw
Iran Bauarbeiten zweiter Reaktor Atomkraftwerk in Buschehr
Picha: Getty Images/AFP/A. Kenare

Katika Mkutano wa mtandaoni uliofanyika Jumatatu wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi zilizosaini mkataba wa nyuklia na Iran, walikubaliana kushughulikia uwezekano wa Marekani kurejea tena katika mkataba huo. Nchi hizo ni pamoja na China Urusi, Ujerumani, Ufaransa na Uingereza.

Katika mazungumzo ya jana Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujermani Heiko Mass amesema mabadiliko ya utawala nchini Marekani yanamaanisha Iran ina nafasi ya mwisho ya maendeleo ambayo haipaswi kupotezwa. Amesema kwa sasa hawataraji kuona makubaliano yakikiukwa kama walivyoshuhudia hivi karibuni huku akionya kuwa hatua kama hizo huenda zikayumbisha zaidi makubaliano hayo ya nyuklia kati ya mataifa yalio na nguvu duniani pamoja na Iran.

Mwenzake wa Uingereza Dominic Raab amesema katika mkutano huo alikuwa wazi kabisa kuionya Iran kutotekeleza upanuzi ulioutangaza hivi karibuni wa mpango wake wa nyuklia. Raab amesema hilo likifanyika basi huenda likadidimiza maendeleo ya Iran yaliotarajiwa kuonekana mwaka 2021.

Kwa upande wake waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Mohammad Javad Zarif ameahidi kupitia ujumbe wake wa twitter kwamba taifa lake litabadili misimamo yake iliyochukua kufuatia Marekani kujiondoa katika mkataba wa nyuklia lakini hilo litafanyika iwapo mataifa yaliosaini mkataba huo pia yatasimamia majukumu yao ipasavyo.

Iran Urananreicherungsanlage Isfahan
Afisa akikagua mojawapo ya kinu cha UraniamuPicha: picture-alliance/dpa/A. Taherkenareh

Waziri Javad Zarif amesema ni lazima watu wa Iran wahisi athari na utulivu wa kuondolewa kwa vikwazo vilivyolenga kuuharibu uchumi wake. Licha ya Iran kukiukwa masharti yaliokubaliwa katika mkataba huo wa nyuklia wa mwaka 2015, shirika la nguvu za atomiki duniani IAEA imeripoti kuwa Iran imeendelea kutoa idhini ya wachunguzi kufikia vinu vyake vya nyuklia ambayo ni makubaliano muhimu katika mkataba wa  JCPOA.

Rais Mteule Joe Biden atakaeingia rasmi madarakani Januari 20 amedokeza kuwa Marekani itajiunga tena na mkataba huo unaofahamika kama mpango wa pamoja wa kuchukua hatua ama (JCPOA) ulionuiwa kuidhibiti dhamira ya Iran kujipatia silaha za nyuklia. Mpango huo umekuwa ukiyumba tangu rais Donald Trump alipoiondoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia mwaka 2018 na kuiwekea Iran vikwazo zaidi vya kiuchumi.

Baada ya Marekani kujiondoa katika mkataba huo wa nyuklia, Iran imekuwa ikikiuka matakwa ya mkataba kwa kuongeza kiwango chake cha urutubishwaji wa madini ya urani katika shughuli zake za nyuklia. Hivi karibuni Iran ilipanga  kuongeza gesi ya urani kwenye mitambo ya kinu chake cha nyuklia, mpango uliokosolewa vikali na Ufaransa Ujerumani na Uingereza