Masikini Japan, temeko na Tsunami yaiwacha nchi vipande vipande! | Masuala ya Jamii | DW | 12.03.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Masikini Japan, temeko na Tsunami yaiwacha nchi vipande vipande!

Maelfu ya walionusurika na mtetemeko mkubwa wa ardhi na mawimbi ya Tsunami, wanasongamana katika maeneo ya kuwahifadhi, huku juhudi za kuwatafuta wahanga wa maafa haya zikiendelea katika maeneo ya mwambao wa nchi hiyo.

Maafa makubwa nchini Japan

Maafa makubwa nchini Japan

Sura katika maeneo hayo ni ya kuitisha na kusikitisha. Magari na maboti yamekwama katika matope.

Picha za kutoka angani zinaonesha majumba na magari moshi yakirushwa juu kama vitu vya kuchezea watoto. Mawimbi makubwa ya maji kutoka baharini yaliyakumba maeneo yanayozunguka mji wa Sendai, kilomita 130 kutoka kwenye kiini cha mtetemeko huo, na moja ya kati ya maeneo yaliyopigwa vibaya sana.

Shahidi mmoja wa mkasa huo alisema aliiona barabara ikienda juu na chini kama mawimbi, majumba yalikuwa yanawaka moto na wakati huo huo theluji ikianguka.

Mripuko kwenye kinu cha nyukliya

Mripuko kwenye viwanda mjini Sendai

Mripuko kwenye viwanda mjini Sendai

Licha ya hayo, miyale ya kinyukliya imevuja kutoka kwenye kinu cha kinyukliya kilichoharibika, huko Fukushima, karibu na Sendai, mji wa bandari wenye wakaazi wapatao milioni moja.

Katika maeneo yaliyo karibu na Fukushima, watu walionusurika walipanga milolongo huku wakipewa maji na chai katika vituo vya mijini, na wanajeshi wa Japan wakiendelea kutafuta wahanga wa maafa haya ya kihistoria.

Mamia ya boti za uvuvi, nyingi zao zilipinduka na kukwama kwenye matope yaliotokana na mawimbi ya Tsunami yaliofikia urefu wa mita kumi. Maelfu ya watu wamebidi wayaache makaazi yao, wengi wakijifunika mablanketi na kukumbatiana mabarabarani.

Hadi sasa, inasemakana si chini ya watu 1,300 wamekufa kutokana na mtetemeko huo wa ardhi nchini Japan, ambao ni wa tano kwa ukubwa kutokea katika nchi hiyo mnamo karne moja iliopita.

Simu za mezani na zile za mikononi hazifanyi kazi katika maeneo mengi ya Japan. Katika mji wa Mito, ambao ni miongoni mwa maeneo yaliyoathirika sana, mamia ya watu wamepiga mistari katika duka kubwa liloharibika, wakingoja kupatiwa madawa, maji na mahitaji mengine. Katika eneo hilo maduka yote yamefungwa.

Mjini Tokyo watu wanaanza kujipanga upya, wakihofia usitokee mtetemeko mwengine mkubwa sawa na ule wa mwaka 1923 ambao uliwauwa watu 140,000.

Kuna baadhi ya watu katika mji huo waliopumua kuona hamna uharibifu mkubwa umetokea katika mji huo, lakini kuna vurugu na mchafukoge, hasa kwa vile inasemakana miale ya kinyukliya imevuja kutoka kwenye kinu cha kinyukliya cha Fukushima.

Ulimwengu waungana na Japan

Kansela Angela Merkel

Kansela Angela Merkel

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, ameahidi kuipa Japan msaada wa muda mrefu ili kuyajenga upya maeneo yalioathirika na mtetemeko huo wa ardhi.

"Nataka kuwaambia watu huko Japan kwamba sisi katika dakika hii ngumu na isiokuwa ya kawaida tunawakumbuka. Kuna watu wengi waliokufa, na bila ya shaka ukumbwa wa balaa hilo utaonekana katika masaa yajayo.

"Tuko tayari kutoa msaada wote tunaoweza. Tayari tumepeleka mabingwa wa uokozi hadi Japan, na Ujerumani itafanya kila inachoweza, sio tu katika siku zijazo, lakini pia katika muda mrefu ujao, kushiriki katika ujenzi mpya wa maeneo yalioharibika." Alisema Merkel hapo jana akiwa mjini Brussels.

Pia Rais Barack Obama wa Marekani, amepeleka salamu zake za pole kwa serikali ya Japan; huku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon akiahidi kuisaidia Japan katika kipindi hiki kigumu.

Licha ya kwamba Wajapani wana vitabu vya kudurusu pale unapotokea mtetemeko wa ardhi, na kila wakati wanafanya mazoezi juu ya kujikinga na balaa zinazofuatana na jambo hilo, lakini kweli mtu anakumbuka kitabu alichosomeshwa wakati mtetemeko unapopiga?

Kila mtu wakati huo hukimbia wakati kila kitu kinapotikisika, na watu huambiwa tu fungeni gesi na moto katika nyumba zenu, lakini mambo hayo wakati huo hayagongi katika ubongo wa mtu.

Waziri Mkuu wa Japan, Naoto Kan, leo amewahimiza wananchi wawe watulivu, hasa wale walioko karibu na kinu cha kinyukliya kilichopigwa na tetemeko la ardhi.

Kan ameapa kuwa serikali yake itafanya kila iwezekanavyo kuhakikisha hakuna mtu hata mmoja atakayesumbuliwa na matatizo ya kiafya.

Waziri wa Mazingira wa Ujerumani, Nobert Röttgen, amesema licha ya matatizo yaliotokana na vinu vya kinyukliya vya Japan, lakini hakuna hatari kwa Ujerumani.

"Kutokana na ujuzi wote tulio nao, haiwezekani kwa miyale ya kinyukliya kuwa na athari hapa Ujerumani. Hii inatokana na masafa makubwa kutoka Japan na pia kutokana na ujuzi tulionao kuhusu hali ya hewa." Alisema Röttgen.

Lakini mabingwa wa mambo wanasema huweza kukatokea na athari za kimazingira katika maeneo yalio karibu na Japan, hasa katika Bahari ya Pasifiki.

Mwandishi: Miraji Othman/Reuters
Mhariri: Mohammed Dahman

DW inapendekeza

 • Tarehe 12.03.2011
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/10Y8j
 • Tarehe 12.03.2011
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/10Y8j
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com