1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashtaka ya Rwanda dhidi ya Ufaransa

Oummilkhheir19 Aprili 2007

Ufaransa yashitakiwa na Rwanda mbele ya mahakama ya kimataifa mjini The Hague

https://p.dw.com/p/CHFu
Mabufuru ya wahanga wa mauwaji ya halaiki ya mwaka 1994
Mabufuru ya wahanga wa mauwaji ya halaiki ya mwaka 1994Picha: AP

Rwanda imeufikisha mzozo wake wa kisiasa na kisheria dhidi ya Ufaransa,mbele ya mahakama ya kimataifa mjini The Hague,baada ya waranti uliotangazwa na Ufaransa dhidi ya wapambe wa rais paul Kagame.

Serikali ya mjini Kigali imetuma mashtaka dhidi ya Ufaransa mbele ya mahakama ya kimataifa ya sheria mjini The Hague-kwa hoja kwamba waranti uliotangazwa na jaji Jean-Louis Bruguière unavunja mamlaka ya Rwanda.

Mwezi November mwaka jana jaji huyo wa Ufaramnsa alitangaza amri ya kukamatwa wapambe tisaa wa rais Paul Kagame kwa kuhusika na kuuliwa mtangulizi wake Juvenal Habyarimana mwezi April mwaka 1994.Wapambe hao ni pamoja na mkuu wa jeshi la Rwanda James Kabarebe,mkuu wa itifaki Rose Kabuye na balozi wa Rwanda nchini India Charles Kayomba.

Tuhuma hizo zimeikasirisha vibaya sana serikali ya mjini Kigali inayozitaja kama njama tuu zilizolengwa kuficha mchango wa Ufaransa katika kuwapatia mafunzo wanajeshi wa Rwanda waliohusika na mauwaji ya halaiki.

Rais Paul Kagame ambae wakati ule alikua akiongoza harakati za wapiganaji wa chini kwa chini dhidi ya serikali iliyokua ikidhibitiwa na wahutu amekua akiwabebesha jukumu la kudenguliwa ndege aliyokua akisafiria Juvenal Habyarimana,maafisa wa kihutu waliokua wakiungwa mkono na Ufaransa.Serikali ya mjini Paris kwa upande wake imekua daima ikikanusha kuhusika kwa aina yoyote na mauwaji ya halaiki ikihoji ilijihusisha na kuwalinda wananchi dhidi dhidi ya wanamgambo wa kihutu.

Ufaransa haitambui moja kwa moja madaraka ya mahakama hiyo ya kimataifa ya mjini The Hague.Hata hivyo waziri wa sheria wa Rwanda Tharcisse KARUGARAMA akifuatana na mwanasheria mkuu Martin Ngoga amewaambia waandishi habari tunanukuu:”Ufaranmsa ina haki ya kuchagua kati ya kuja na kutokuja…ikiwa wanayosema ni ya dhati na hayakushawishiwa kisiasa-basi wangebidi waje mbele ya mahakama isiyopendelea upande wowote.

Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Ufaransa haijasema chochote kuhusu mashtaka hayo ya Rwanda.

Wadadisi wanasema hakuna uhakika kama Ufaransa itajibu mwaliko kabla ya mahakama kuamua kufungua kesi au la.

Hadi uamuzi wa mahakama utakapopitishwa,rais Kagame ameshauri waranti hizo zisitishwe kwanza.

Itafaa kusema hapa kwamba waranti hizo na dhana za jaji Brugières dhidi ya rais Paul Kagame ndio chanzo cha Rwanda kuvunja uhusiano wa kibalozi pamoja na Ufaransa,mwishoni mwa mwezi November mwaka jana.