1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HALI MBAYA UKANDA WA GAZA

Mtullya, Abdu Said6 Machi 2008

Hali inayowakabili wapalestina wa Ukanda wa Gaza imezidi kuwa mbaya.

https://p.dw.com/p/DJQm
Wapalestina wa Ngaza wanaokabiliwana vikwazo vya Israel.Picha: AP


Mashirika yanayotetea haki za binadamu yamesema  hali  inayowakabili watu kwenye Ukanda wa Gaza imefikia kiwango kibaya, kisichokuwa  na mithili tokea sehemu hiyo ianze kukaliwa na Israel mwaka 1967.

Mashirika hayo yameripoti kuwa watu wanaothirika  kutokana na hali hiyo ni pamoja na watoto wa shule.


Madai hayo yametolewa pia na mashirika ya misaada ya Uingereza na yameutaka Umoja wa Ulaya uanze mazungumzo na viongozi wa chama cha Hamas wanaoongoza kwenye Ukanda wa Gaza.

Asasi za kutetea haki za binadamu pamoja na mashirika hayo ya misaada pia  yameilaumu Israel kwa kuwawekea vikwazo wapalestina wa Ukanda wa Gaza na kuchukua hatua za kijeshi zinazochochea moto zaidi.

Katika ripoti  yao mashirika hayo yamesema Israel inawaadhibu wapalestina wote wanaoishi kwenye Ukanda wa Gaza ikiwa pamoja na watoto wa shule.

Ripoti imesema  hali inayowakabili wapalestina milioni moja na laki tano katika sehemu hiyo imefikia hatua mbaya   isiyokuwa na mithili tokea sehemu hiyo  ianze kukaliwa na Israel mwaka 1967.


Katika ripoti hiyo mashirika manane yisiyokuwa ya kiserikali yamesisitiza umuhimu wa kufanyika mazungumzo na viongozi wa Hamas waliotwaa mamlaka ya Ukanda wa Gaza mwezi juni mwaka jana ambao  wanatathminiwa kuwa magaidi na Umoja wa Ulaya,Marekani na Israel.

Asasi za kimataifa  zimelalamika kwamba   jumuiya ya kimataifa inawatenga   wapalestina wa Ukanda wa Gaza. Wawakilishi wa asasi hizo wameeleza  katika ripoti yao kuwa sera ya kuwatenga wapalestina haijaleta manufaa kwa yeyote Wameutaka Umoja wa Ulaya uachane na sera hiyo na uanze mazungumzo na  wawakilishi wote wa wapalestina.


Maisha ya wapalestina kwenye Ukanda wa   Gaza  yamezidi kuwa mabaya kutokana  na hatua ya Israel kuwabana wapalestina hao kwa vikwazo ,ikiwa ni njia mojawapo ya kuzuia mashambulio ya roketi yanayofanywa na wapiganaji wa kipalestina dhidi ya Israel, lakini mashirika   hayo yamedai katika ripoti yao kuwa hatua za Israel haziongezi usalama kwa wapalestina wala kwa waisraeli wenyewe. na kutokana na hayo mashirika hayo ya  misaada  yameutaka Umoja  wa Ulaya  utoe kauli kali kulaani hatua za Israel za kuendelea kuwabana wapalsetina wa   Ukanda wa Gaza kwa vikwazo na  kuwazingira watu hao.


Hali ya Ukanda wa Gaza  imekuwa mbaya  kiasi  kwamba  asilimia 80 ya watu wanategemea msaada wa chakula kutoka  nje na asimilia 40 ya watu hawana ajira.

Kutokana na vikwazo spea, haziingii Ukanda wa Gaza na kutokana hali hiyo hospitali haziwezi kuendesha mashine za kuokolea maisha ya watu.

Watoto wa shule pia hawapati vitabu kutokana na vikwazo vya Israel.

Mashirika ya kimataifa yamesema  ikiwa vikwazo havitaondoshwa,  wapalestina wa Ukanda wa Gaza watakabiliwa na maafa makubwa zaidi.


Mashirika ya kimataifa yamesema hali imezidi kuwa mbaya kutokana na hatua za kijeshi zilizoanza kuchukuliwa mwezi februari na Israel ili kuzuia  mashambulio ya roketi.

Tokea wakati huo wapalestina zaidi ya 120  wameuliwa na majeshi ya Israel ikiwa pamoja na watoto 20.