1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashirika ya misaada yaonya juu ya baa la njaa Pembe ya Afrika

Halima Nyanza11 Agosti 2011

Mashirika ya misaada yameonya kwamba janga la njaa lililoikumba eneo la pembe ya Afrika litaongezeka iwapo mvua zinazotarajiwa Mwezi Oktoba hazitanyesha na kuitahadharisha Marekani kutopunguza misaada kipindi hiki.

https://p.dw.com/p/12EzJ
wanawake na watoto katika foleni ya chakulaPicha: AP

Takriban watu milioni mbili katika maeneo ya pembe ya Afrika yaliyokumbwa na ukame wameathiriwa vibaya na baa la njaa lililokumba baadhi ya maeneo ya nchi zaKenya, Ethiopia, Djibouti na Somalia.

Wasiwasi huo wa kuongezeka kwa baa hilo unakuwa wakati ambapo kamati ya bunge la Marekani inayohusika na masuala ya kuratibu fedha za misaada ikipendekezwa kupunguziwa bajeti kwa Shirika la misaada la Kimataifa la Marekani -USAID-  kwa mwaka wa fedha wa 2012 kwa kiasi cha dola za nchi hiyo milioni 488 kutika kiwango cha mwaka uliopita na dola milioni 705 pungufu ya ilivyopendekeza serikali ya Rais Barack Obama.

Hungernde Äthiopier in Wadla
Waethiopia wakisubiri msaada wa chakulaPicha: AP

Mkuu wa Utawala msaidizi wa shirika hilo la misaada la Marekani Donald Steinberg amesema iwapo bajeti yao itapunguzwa katika kutoa msaada wa chakula kutatokea madhara.

Mpaka sasa Marekani imetoa kiasi cha dola milioni 570 kupambana na baa la njaa katika eneo la pembe ya Afrika. 

Wakati hali hiyo ya wasiwasi ikijitokeza, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani -WFP- limesema mashirika ya misaada yanashindwa kuwafikia zaidi ya Wasomali milioni mbili katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi na baa la njaa kutokana na kundi la wapiganaji la Al Shabaab kuyazuia mashirika mengi ya misaada yasifike katika maeneo hayo.

Hata hivyo hali katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu imekuwa na afueni, ambapo Msaidizi wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia misaada ya dharura Valerie Amos kusema kwamba idadi ya wakimbizi wa Kisomali  wanaokimbili nchini Somalia imepingua tangu wapiganaji wa Al Shabaab kujiondoa katika mji mkuu huo, mwishoni mwa wiki na kufungua njia kwa misaada zaidi kuwafikia walengwa.

Amesema watuwapatao laki moja wameyakimbia maeneo ya kati na kusini mwa nchi hiyo na kukimbilia Mogadishu. Hata hivyo ameonya kwamba hali ya usalama bado siyo nzuri.

Wahlen in der Türkei Recep Tayyip Erdogan
Waziri Mkuu wa Uturuki, Tayyip ErdoganPicha: picture alliance/dpa

Katika hatua nyingine Waziri mkuu wa Uturuki Tayyip Erdogan amearifu kwamba atayatembelea maeneo yaliyokumbwa na baa la njaa nchini Somalia akiwa pamoja na familia yake katika siku zijazo. Katika ziara hiyo pia atakuwemo Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Uturuki. Imekuwa nadra sana kwa viongozo duniani kuitembelea nchi hiyo kutokana na kukosa usalama.

Waziri mkuu wa Uturuki amesema ziara hiyo itakuwa ni ya kujionea wenyewe jinsi hali ilivyo katika taifa hilo lisilo na usalama duniani.

Baa la njaa nchini Somalia limesababisha asilimia 10 ya watoto nchini humo walio na umri chini ya miaka 10 kufariki dunia kila baada ya wiki 11.

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia misaada Catherine Bragg ameelezea juu ya kina mama wanavyolazimika kuwaacha watoto wao wachanga wakifa njiani, wakati wanapotembea kwa wiki nyingi wakitafuta usalama.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa anayehusika na  Somalia Augustine Mahiga amesema karibu  watu milioni 3.7,nusu ya idadi ya jumla Wasomali,  wako katika hatari ya kukumbwa na baa la njaa.

Mwandishi: Halima Nyanza(afp,Reuters,dpa)

Mhariri:  Mohammed Abdulrahman