1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashindano ya 11 ya riadha duniani

Ramadhan Ali24 Agosti 2007

Wanariadha kutoka nchi 203 wanaania kuanzia leo hadi Septemba 2 medali za dhahabu,fedha na shaba mjini Osaka,Japan.Miongoni mwao wale wa Kenya,Ethiopia,Tanzania na Uganda.

https://p.dw.com/p/CHbA

Mashindano ya riadha ulimwenguni –World Athletics Championsships-yananza leo (jumamosi) mjini Osaka,Japan tena kwa mshindo mkubwa:Medali 3 za dhahabu zinaaniwa katika mbio za marathon –wanaume ambamo wakenya,waethiopia na wenyeji wajapani, watazamiwa kutia fora.

Mita 10.000 wanawake ambamo msichana wa Ethiopia Tirrunesh Dibaba, anatapia kuwa mwanariadha wa kwanza kushinda masafa hayo kwa mara ya pili mfululizo.Medali ya tatu ya dhahabu inaaniwa katika kurusha gololi la chuma (shot-put).

Jumla ya wanariadha 3000 kutoka nchi 203 wanashiriki kuanzia leo hadi septemba 2na hii ni rekodi inayopita ile ya Seville,Spain,miaka 8 nyuma:

Medali ya kwanza ya dhahabu inayoweza kwenda barani afrika asubuhi ya leo itatoka katika mbio ndefu za marathon:Lakini kwa kuwa bingwa wa dunia Jaouad Gharib hatakuwapo barabarani kwa kuwa ameumia, mlango uwazi kwa mzaliwa wa Kenya Mbarak hassan Shami kuwatilia wakenya kitumbua chao mchanga.

Kwani,atakimbia leo akipepea bendera ya Qatar na sio ya Kenya alikozaliwa.Mbarak amewasili Osaka akiwa ameshinda mbio zote 5 za marathon tangu alipoingia katika medani yam bio hizi 2005.Aliwika katika michezo ya asia-Asian Games desemba mwaka jana na mbio za Paris marathon kwa muda bora msimu huu wa masaa 2:07.19.

Lakini wanariadha 11 kati ya 23 bora kabisa watakaotimika leo mbio mjini Osaka,wamevuka muda wa saa 2 na dakika 8 na pamoja nao ni mkenya William Kiplagat na Hendrick Ramala wa afrika Kusini.

Katika finali nyengine hii leo –mita 10.000 wanawake,bingwa mara 2-mita 5000 na 10.000 wa dunia,muethiopia Tirunesh Dibaba amejiwinda alaasiri ya leo kuwaongoza waethiopia wenzake kutamba tena katika masafa hayo.Dibaba anatazamia mbio za leo kuwa ngumu kama zile za miaka 2 nyuma alizoshinda mjini Helsinki,Finland.

Mwaka 2005 huko Helsiniki,Dibaba alishinda kwa kumpiku mwenzake Berhane Adere na dada yake mkubwa Ejageyehu Dibaba akija 3.Hivyo alikuwa mwanamke wa kwsanza kunyakua mataji yote 2 –mita 5000 na 10.000 katika mashindano yale yale.

Katika masafa ya mita 5000 wiki ijayo,Dibaba itambidi kumtimua nje muethiopia mwenzake Meseret Defar ili anyakue taji hilo kwa mara ya 3 ikiwa ni rekodi.

Kuna muethiopia mwengine-Tufa ambae ndie aliekimbia muda bora msimu huu.Mkenya Florence Kiplagat amekimbia muda wapili bora mwaka huu.

Uwanjani leo ni changamoto ya duru ya kwanza ya mita 100 wanaume:Hapo ataamuliwa nani binadamu wa kasi duniani na mahasimu 2-bingwa wa rekodi ya dunia Asafa Powell wa Jamaica, anakutana kwa mara ya kwanza na chipukizi wa Marekani Tyson Gay.Wote 2 wana duru mbili kabla finali ya kesho jumapili.Na wanasema wanapopambana mafahali 2, zimiazo ni nyasi.

Hali itakua hivyo, kwani Gay ameazimia kuifuta rekodi ya Powell; na Powell ataka kurudi Kingston,Jamaica na medali ya dhahabu.Kwa kweli, Tyson Gay analenga kutwaa medali 3 za dhahabu katika mashindano haya-kutoka mita 100/200 na katika mita 100X4 kupokezana.Asafa ana rekodi ya dunia.

Mashindano haya ya Osaka,Japan, ni ya kujinoa kwa mashindano ya olimpik mwakani mjini Beijing,China.Na mshindi wa Osaka aweza kijitapa kuwa ndie atakaekuwa wa Olimpik mwakani.

Halmashauri kuu ya olimpik ulimwenguni-IOC, imeshaonya kwahivyo, kuwa mwanariadha yeyote atakaefanya madhambi ya doping-matumizi ya madawa kuongeza kasi,atapigwa marufuku kushiriki katika michezo ya Olimpik ya mwakani.