1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashauriano ya "Mdahalo wa Petersburg juu ya Ushirika baina ya Ujerumani na Russia"

Othman, Miraji3 Oktoba 2008

Mitizamo tafauti kuhusu Ushirika baina ya Ujerumani na Russia

https://p.dw.com/p/FTWE
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani akizungumza na Rais Medvedev wa Russia katika mji wa St. PetersburgPicha: AP

Ushirika baina ya Ujerumani na Russia ni mananeo matamu yaliosikika mwaka huu katika mashauriano ya kila mwaka baina ya nchi hizo mbili yaliopewa jina la Mdahalo wa St. Petersburg. Pale wanasiasa, wafanya biashara na wawakilishi wa jamii kutoka nchi hizo mbili wanapokutana, basi huwa wazi zaidi vipi maslahi ya pamoja baina ya nchi mbili hizo yanavofungamana. Uzito hutiliwa juu ya namna ya kuowanisha maslahi ya Russia ilio na utajiri wa mali ghafi na Ujerumani ambayo ni nchi ya kiviwanda. Mdahalo wa St. Petersburg ulikuwa na kauli mbiu: Ushirika katika kuzifanya ziwe za kisasa kabisa Russia na Ujerumani.


Licha ya kwamba watu wanaweza kukubaliana juu ile fikra ya kimsingi ya kuwa na jamii ya kisasa, lakini msamiati huo hupewa tafsiri tafauti. Kwa upande wa Russia, wao neno usasa hasa lina maana ya jamii kuwa na uchumi na teknolojia ya kisasa, kwa mfano kuzidisha na kuboresha uzalishaji wa nishati na kuvumbua teknolojia ya kuvifanya vipuri kuwa vidogo, lakini kuwa na uwezo mkubwa wa kufanya kazi. Kwa upande wa Ujerumani, miradfi kama hiyo haikataliki hata kidogo.

Lakini kwa Ujerumani, wao neno usasa lina majukumu yalio mapana na ya ujumla zaidi; linaingiza pia jamii kujifungua, dola kuwa wazi kuhusu matendo yake, na zaidi linajumuisha pia kujenga dola ilio na msingi wa utawala wa sheria. Mambo hayo, kwa mujibu wa maneno ya wawakilishi wa tabaka ya juu ya Russia, sio kwamba yanakatalika kabisa. Lakini, hata hivyo, wao hawajuwi hasa nini kilicho nyuma ya misamiati hiyo. Mara nyingi na kwa haraka Warussia wanayaona misamiati hiyo kama jaribio la wao kulishwa maneno vinywani mwao, kuwa yuko juu yao mwalimu mkuu wa shule anayewasomesha nini la kufanya na lisilofaa kutenda, na pia kuingiliwa katika mambo yao ya ndani.

Sio tu kwamba neno usasa linaangaliwa kwa sura tafauti baina ya watu wa Ujerumani na Russia, lakini pia neno hilo limetathminiwa tafauti tangu kusambaratika ile iliokuwa Urussi, yaani mambo yameachwa kuangaliwa kwa jicho zuri tangu wakati huo wa 1989 hadi 1991. Urussi, iliokuwa dola kuu, mara ikajikuta imepoteza maeneo iliokuwa na ushawishi, hasa Ulaya ya Mashariki na ya Kati, na pia katika maeneo yaliokuwa hapo kabla yanaipendelea Urussi. Kwa mtizamo wa Russia hali ya kwenda chini siasa ya kigeni ya Russia wakati huo imepelekea kujitanua taasisi za nchi za Magharibi, kama vile Umoja wa Ulaya na kambi ya Kujihami ya NATO, katika maeneo ambayo hapo zamani yalikuwa chini ya ubwana wa Warussia.

Hali hiyo inaonekana huko Russia kuwa ni kitisho, jambo linalopelekea kuweko nchini humo misimamo mikali ya kuipinga Marekani, na kupelekea pia lile jibu la Russia huko Georgia, ili kwamba isipoteze maeneo zaidi ambayo kiasili imeyaona kuwa ni maeneo yake ya ushawishi. Na ndio maana kuna hii jitihada ya Russia kutaka kuweko mkataba juu ya usalama wa pamoja barani Ulaya, angalau kuhakikisha kwamba kila upande unatambua maeneo ya ushawishi ya upande mwengine.

Hapa Ujerumani inatambulika kwamba ilikuwa sio rahisi kwa Russia kuinywa ile shubiri kwamba imepoteza ile hadhi yake ya kuwa dola kuu. Wakati huo huo, Wajerumani wanauona wakati baina ya mwaka 1989 na 1991 kuwa ni wakati mzuri, ukitilia maanani kwamba wakati huo Ujerumani iliungana tena hapo Oktoba 3, na hivyo kukaribisha kusambaratika kwa utawala wa Urussi na wa Russia, jambo lilionekana kwamba litaweza kufungua njia ya kuweko uhuru na demokrasia katika Ulaya Mashariki na katika dola zilizokuwemo katika Shirikisho la Urussi. Kutanuka kwa taasisi za nchi za Magharibi hadi Mashariki ya Ulaya kulichukuliwa kuwa ni kuuendeleza ule mradi wa Ulaya wa kusambaza neema na uhuru katika amani, hali ambayo itaweza kuziingiza pia Ukraine, Georgia na nchi nyingine. Kutokana na msingi huo, ndio maana Kansela Angela Merkel wa Ujerumani analiona jibu la Russia kuhusu mzozo uliotokea katika eneo la Milima ya Kaukas lilikuwa ni kali mno, kuvuka mipaka, na anashikilia kwamba ardhi ya Georgia irejee kama ilivokuwa, jambo ambalo halijakubalika kwa upande wa Warussia.

Vizingiti hivi vyote viliwili vilivyo na mizizi inayokwenda chini, pale unapoziangalia juhudi za kuendeleza ushirika, havijaweza kuondoshwa katika mashauriano haya ya mwaka huu ya Mdahalo baina ya Ujerumani na Russia. Hata hivyo, jambo moja ni wazi: Bila ya mazungumzo vizingiti hivyo havitaondoshwa.