1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi ya kuwaondoa IS yaendelea Iraq na Syria

Grace Kabogo
10 Novemba 2016

Vikosi vinavyoungwa mkono na Marekani vimeongeza mashambulizi dhidi ya ngome muhimu zinazodhibitiwa na wapiganaji wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu-IS, nchini Syria na Iraq.

https://p.dw.com/p/2SSWY
Irak Kampf um Mossul gegen den IS
Picha: picture-alliance/Anadolu Agency/H. Baban

Wakisaidiwa na mashambulizi ya anga ya muungano wa majeshi yanayoongozwa na Marekani, vikosi vya Iraq vimezidi kusonga mbele kuingia Mosul, ngome kuu ya IS, huku muungano wa wapiganaji wa Kikurdi wakielekea Raqqa, Syria, mji ambao ni ngome kuu ya wapiganaji hao wa jihadi.

Shirika linalofuatilia haki za binaadamu nchini Syria lenye makao yake mjini London, Uingereza, limesema vikosi vya anga jana usiku, vimeshambulia kijiji cha Al-Heisha kinachodhibitiwa na IS, ambacho kiko umbali wa kilomita 40 kaskazini mwa Iraq.

Mkurugenzi wa shirika hilo, Rami Abdul Rahman, amesema mashambulizi ya Raqqa yamesababisha mauaji ya raia 20, huku wanawake wanane na watoto wawili wakiwa miongoni mwa waliouawa na wengine 32 wamejeruhiwa. Hata hivyo, msemaji wa vikosi vinavyopigania demokrasia nchini Syria-SDF, ambavyo vinaungwa mkono na Marekani, Jinah Sheikh Ahmed, amekanusha kutokea kwa mauaji hayo ya raia na kwamba madai yoyote kama hayo yanatolewa na IS.

Syrien SDF PK Sturm auf Rakka
WAnajeshi wa vikosi vya SDFPicha: Getty Images/AFP/D. Souleiman

Msemaji wa muungano wa majeshi unaoongozwa na Marekani, Kanali John Dorrian amesema inaonekana kuwa mashambulizi yamefanyika kwenye eneo hilo. Amesema baada ya kufanyika tathmini ya awali, muungano huo umethibitisha kwamba ulifanya mashambulizi kwenye eneo ambalo limeelezwa. Hata hivyo, panahitajika taarifa zaidi zitakazoonyesha hitimisho kwamba wahanga wa mashambulizi hayo ni raia. Kwa mujibu wa vikosi vya SDF, kiasi ya familia 200 zimekikimbia kijiji cha Al-Heisha.

Mashambulizi yalianza Jumamosi

Siku ya Jumamosi vikosi vya usalama vya Iraq, vilianzisha operesheni yenye lengo la kuwafurumusha wapiganaji wa IS, kutoka kwenye mji wa Mosul. Taher Farhan, afisa polisi wa shirikisho la Iraq amesema ushindi utapatikana hivi karibuni.

''Tunakaribia kushinda, tuna matumaini kwamba umebaki muda kidogo tu hadi tutakapokamilisha kazi ya kuikomboa Mosul. Sasa tuko Hammam al-Alil, tunashukuru Mungu tumeweza kulisafisha eneo hili na kama mnavyoona familia zimerudi hapa,'' alisema Farhan.

Syrien Rakka U.S. Soldaten
Wanajeshi wa Marekani wanaosaidia mashambulizi ya Iraq na SyriaPicha: Reuters/R. Said

Wakati huo huo, Shirika la kimataifa la haki za binaadamu, Amnesty International limesema vikosi vya serikali vya Iraq vinawatesa na kuwaua wanakijiji wa kusini mwa Mosul. Hiyo ni ripoti ya kwanza kutolewa kuhusu ukiukwaji wa haki za binaadamu tangu kuanza kwa mashambulizi ya kuukomboa mji wa Mosul kutoka kwa IS.

Shirika hilo limesema wahanga ni pamoja na watu sita waliogunduliwa mwezi uliopita kwenye wilaya ndogo za Shura na Qayyara, ambazo vikosi vya usalama vinashuku vina mafungamano na kundi la IS ambalo liliutwaa mji huo mwaka 2014. Hata hivyo, msemaji wa jeshi la polisi la Iraq na wizara ya mambo ya ndani, hakuweza kupatikana mara moja kuzungumzia madai hayo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, AP, Reuters
Mhariri: Caro Robi