MASHAMBULIZI YA CHACHA GAZA | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 05.01.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

MASHAMBULIZI YA CHACHA GAZA

Majeshi ya Israel yameendeleza mashambulizi yake dhidi ya wapiganaji wa kundi la hamas katika ukanda wa gaza na kufikisha idadi ya wapalestina waliofariki kufuatia mashambulizi hayo zaidi ya 515.

Majeshi ya Israel yakifanya mshambulizi Kusini mwa Ukanda wa Gaza

Majeshi ya Israel yakifanya mshambulizi Kusini mwa Ukanda wa Gaza


Ni siku ya kumi tangu Israel kuanzisha mashambulizi dhidi ya wapiganaji wa kundi la hamas katika ukanda wa gaza,na maafa zaidi yameendelea kuripotiwa. Usiku wa kuamkia leo majeshi ya Israel yamefanya zaidi ya mashambulizi 30 ya angani, yakilenga hasa misikiti na makaazi ya viongozi wa kundi la hamas.Majeshi ya Israel yameweza kupenya zaidi katika ukanda wa gaza na kwa sasa vifaru vyao vinaelekea kusini mwa mji wa Khan Younis.


Madaktari wa kipalestina wamesema watoto watano wameauwa usiku wa kuamkia leo katika mashambulizi mawili tofauti. Mashambulizi hasa yamechacha katika eneo la kaskazini karibu na Jabaliya na Beit Lahiya.Majeshi ya Israel pia yameuzingira mji mkuu ulio mashariki na kusini mwa ukanda wa gaza.


Waziri wa ulinzi wa Israeli, Bw Ehud Barak, akizungumza na waandishi wa habari ameeleza kuwa lengo la operesheni inayoendelea ni kuwamaliza wanamgambo wa Hamas.


"mashambulizi yanaendelea kama yalivyopangwa.Si jambo rahisi na halitawahi kuwa jambo rahisi. Lakini tutaendelea kupenya kiasi tuwezavyo.na kama nilivyosema awali, katika kiwango kitakachohitajika.”


Yakaribia wapalestina 75 wameauwa kufuatia mashambulizi hayo tangu siku ya jumamosi,wakati majeshi ya israel yalianza kuimarisha mashambulizi yake dhidi ya wapiganaji wa hamas katika ukanda wa gaza, kwa kuwapeleka wanajeshi wake wa miguu katika eneo hilo lilo na idadi kubwa ya wapalestina.


Israel imeripoti kuwa mwanajeshi wake mmoja alifariki kufuatia kombora na wengine 55 kujeruhiwa tangu walipoanzisha mshambulizi yake ya nchi kavu.Katika kipindi sawa na hicho wapalestina 517 wameuwa wakiwemo watoto 87.

Zaidi ya wengine 2,500 wamejeruhiwa wengi wao wakiwa na majeraha mabaya.


Mashirika ya kutoa misaada yamesema mashambulizi hayo yamesababisha mzozo wa kiutu kwa wenyeji millioni 1.5 wa ukanada wa gaza. Wengi wa wenyeji hao hutengemea msaada wa kigeni baada ya Israel kuuzingira tangu kundi la hamasa kuchukua usimamizi wake mwezi juni mwaka 2007.


Wenyeji wa ukanda wa Gaza kwa sasa kiwango cha umeme kimepungua,hawana maji na wanakabiliwa na upungufu wa chakula.Mahospitali yamekuwa yakihudumu kwa kutumia majenereta.


Serikali ya Israel imekuwa ikipinga shinikizo la jamii ya kimataifa kusitisha mashambulizi katika ukanda wa gaza,haya yakiwa mashambulizi mabaya zaidi kuwahi kufanywa na taifa hilo tangu yale ya mwaka 2006 dhidi ya Lebanon.


Wakati huo huo kundi la Hamas linapanga kutuma ujumbe wake nchini Misri hii leo kwa ajili ya mazungumzo ya kwanza ya kidiplomasia tangu kuanza kwa operesheni ya kijeshi ya Isreali katika ukanda wa gaza.


 • Tarehe 05.01.2009
 • Mwandishi Jane Nyingi
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GSC3
 • Tarehe 05.01.2009
 • Mwandishi Jane Nyingi
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GSC3
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com