1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi dhidi ya waasi kuendelea Ukraine

30 Mei 2014

Ukraine inadai kwamba imeyakombowa maeneo mengi yaliokuwa yakishikiliwa na waasi mashariki mwa nchi wakati serikali ya Marekani ikielezea wasi wasi wake juu ya kuonekana kwa wapiganaji kutoka Chechnya miongoni mwa waasi.

https://p.dw.com/p/1C9dG
Wanajeshi wa Ukraine karibu na Slavyansk. (30.05.2014)
Wanajeshi wa Ukraine karibu na Slavyansk. (30.05.2014)Picha: picture-alliance/AP

Kaimu waziri wa ulinzi wa Ukraine Mykhailo Koval amewaambia waandishi wa habari kwamba jeshi la nchi yake litaendelea na mashambulizi dhidi ya waasi mashariki ya nchi hiyo katika kile wanachokiita operesheni dhidi ya ugaidi licha ya madai ya Urusi ya kutaka kusitishwa mara moja kwa hatua hizo za kijeshi.

Serikali ya Ukraine na washirika wake wa mataifa ya magharibi kwa muda mrefu wamekuwa wakiishutumu Urusi kwa kuchochea uasia huo wa wiki saba ambao umetibuwa misingi ya taifa ya la Ukraine.

Uasi wakanusha mgawanyiko

Kwa upande wao waasi wamepuuza tetesi kwamba kuna mgawanyiko miongoni mwao baada ya wanamgambo kadhaa wenyeji kutimuliwa katika ngome yao ya Donetsk na kikosi cha kijeshi kinachoundwa kwa kiasi kikubwa na Wachechnya na Warusi kutoka eneo tete la Caucasia ya Kaskazini.

Kamanda wa eneo la Donetsk Denis Pushilin amekanusha leo hii kwamba kumefanyika mapinduzi miongoni mwa waasi hao.Amekaririwa na mashirika ya habari ya Urusi akisema viongozi wote wa awali wa uasi huo wataendelea kubakia pale pale.

Kiongozi wa Jamhuri ya Donetsk Denis Pushilin (katikati) mwenye kipaza sauti.
Kiongozi wa Jamhuri ya Donetsk Denis Pushilin (katikati) mwenye kipaza sauti.Picha: DW/F. Warwick

Amesema kile walichokifanya ni kuwaondowa watu wachache wasiokuwa na uadilifu ambao wamehusika na vitendo vya uhalifu ambavyo vinaathiri maslahi ya Jamhuri ya Donetsk.

Wachechnya wapigana Ukraine

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amesema kuonekana hivi karibuni kwa Wachechnya huko Donetsk na Luhansk ni jambo la hatari ambalo Rais Vladimir Putin wa Urusi anapaswa kulishughulikia kwa haraka.

Amesema "Tunatumai Urusi itajishughulisha kwa vitendo zaidi kujaribu kupunguza mvutano,kutumia fursa ya uchaguzi uliofanyika Ukraine na kujenga njia ya kusonga mbele ambapo Ukraine inakuwa daraja kati ya mataifa ya mashariki na magharibi."

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry.
Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry.Picha: Reuters

Wakati huo huo Shirika la Usalama na Ushirikiano Barani Ulaya OSCE limesema leo hii limepoteza mawasiliano na timu yake ya pili ya waangalizi wanne wa kimataifa mashariki mwa Ukraine.

Shirika hilo limesema halikupata taarifa yoyote kutoka timu hiyo ilioko eneo la viwanda la Luhansk tokea Alhamisi jioni wakati liliposimamishwa na watu wenye silaha katika kituo cha ukaguzi barabarani katika mji wa Severodonetsk.

Shirika hilo limesema waangalizi wao wa timu nyengine waliokuwa wakishikiliwa na waasi katika jimbo la Donetsk bado hawakuachiliwa.

Mwandishi :Mohamed Dahman/AFP

Mhariri: Yusuf Saumu